Ahoji kuhusu wahusika kunyimwa dhamana
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee Ibrahim.
Agizo la mahakama hiyo lilitolewa jana na Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Fatma Hamid Mahmoud.
Jaji Fatma alitoa uamuzi huo baada ya kukamilisha kusikiliza pande
mbili kuhusu hatua ya dhamana ya washtakiwa hao 10 kufungwa na DPP kwa
kutumia sheria ya Usalama wa Taifa ibara ya 19 (3) d sura ya 47 ya mwaka
2002.
Jaji Fatma alisema kwamba baada ya kupitia kumbukumbu za mwenendo
wa kesi ya msingi, anaona upande mmoja dhamana imefungwa, lakini bado
upande wa pili anaona dhamana iko wazi dhidi ya washtakiwa hao.
“Upande wa DPP muwasilishe kwa maandishi sababu zenu kwa nini
washtakiwa wasipewe dhamana ndani ya wiki mbili,” alisema Jaji Fatma.
Aidha, alisema kwamba dhamana ni haki ya mshtakiwa na hatua ya
kutolewa sababu ya dhamana hiyo kufungwa itaisaidia mahakama kupata
mwongozo mzuri kabla ya kutoa uamuzi. Kuhusu kesi ya msingi, Jaji Fatma
alisema kwamba itaendelea kusikilizwa kama kawaida licha ya upande wa
mashtaka kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kupinga
uamuzi wa Jaji Abraham Mwampashi juu ya uamuzi wake wa kufuta maamuzi
yote yaliyotolewa na Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar na kuungana na
uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka wa kufunga dhamana.
“Pamoja na upande wa mashtaka kukata rufaa bado hakuzuii Mahakama
Kuu kusikiliza kesi ya msingi na tutaendelea kama kawaida baada ya
kupokea sababu za DPP kufunga dhamana ya washtakiwa,” alisema Jaji
Fatma.
Alisema kwamba suala la kukata rufaa ni haki ya msingi ya kila mtu
kikatiba na kwamba hakuna sababu za msingi za kesi hiyo kusimama
kusubiri maamuzi ya mahakama ya juu.
Kutokana na hali hiyo, Jaji aliutaka upande wa mashtaka uwasilishe
kwa maandishi hoja za DPP kabla ya kesi hiyo kutajwa tena April 10,
mwaka huu.
Awali Mwendesha Mashtaka kutoka ofisi ya DPP, Raya Mselem Issa,
alidai kwamba taratibu za kukata rufaa tayari zimekamilika na kuomba
mahakama kutojadili ombi la dhamana na kuitolea uamuzi hadi Mahakama ya
Rufaa itakapotoa uamuzi wake.
“Ombi letu kesi isimamishwe hadi Mahakama ya Rufaa itakapotoa
mwongozo, rufaa tuliyoikata kwa ajili ya kupinga maamuzi ya Jaji
Mwampashi ya Machi 11, mwaka huu,” alidai Mselem. Katika kesi hiyo,
upande wa mashtaka tayari umekwisha kutaarifu mahakama kuwa upelelezi wa
kesi hiyo umekamilika.
Kesi hiyo inawahusu viongozi 10 wa Uamsho akiwamo Sheikh Farid Hadi
Ahmed, Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, Azzan Khalid Hamdan,
Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakari Suleiman,
Gharib Ahmada Omari, Abdallah Said Ali na Fikirini Majaliwa Fikirini.
Washtakiwa hao wamefunguliwa mashtaka ya uharibifu wa mali za
serikali na kuhatarisha usalama wa taifa kinyume cha kifungu cha 3 (d)
cha sheria ya Usalama wa Taifa sura ya 47 ya mwaka 2002 na kutoa lugha
za uchochezi kinyume cha kifungu cha 11 cha sheria ya Usalama wa Taifa
sura ya 47 ya mwaka 2002.
CHANZO:
NIPASHE