Mbunge wa Jimbo la Ubungo John Mnyika ametoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kueleza sababu za kutokutekelezwa mpaka sasa kwa ahadi zake alizotoa mwaka 2010 za ujenzi wa Machinga Complex na jumba la viwanda vidogo katika jimbo hilo kuchangia katika kupanua wigo wa ajira kwa vijana.
Mnyika aliyasema hayo akijibu swali la mwakilishi wa vijana katika
mkutano wake na wananchi alioufanya katika ofisi za Serikali ya Mtaa wa
Muungano katika kata ya Manzese uliofanyika mwishoni mwa wiki
(16/03/2013).
Mwakilishi huyo wa vijana alitaka kufahamu hatua ambazo mbunge amechukua
kufuatilia kuhusu maeneo ya kufanyia biashara kwa ajili ya
wafanyabiashara wadogo katika jimbo la Ubungo.
“Kazi ya mbunge ni kuwawakilisha wananchi na kuisimamia serikali ili
kuwezesha utatuzi wa kero, matatizo ya maeneo ya wafanyabiashara ndogo
ndogo yamedumu kwa muda mrefu kutokana na udhaifu katika mipango miji na
hivyo maeneo ya wafanyabiashara na masoko kuuzwa, kuvamiwa au kuwa
machache. Nimefuatilia suala hili, kuna ambao wamepata maeneo na wengine
wengi bado”, alijibu Mnyika.
Mbunge alieleza kuwa katika mwaka 2011/2012 alikutana na ‘wamachinga’ wa
jimbo la Ubungo hatua iliyosababisha kamati maalum inayohusisha
wafanyabiashara na Manispaa kuundwa kwa ajili ya kuwezesha
wafanyabiashara wa Ubungo kupatiwa maeneo katika masoko yaliyotengwa.
Mnyika alisema kwamba atashirikiana na madiwani mwaka huu wa 2013
kutathmini kazi iliyofanywa na kamati hiyo ili kuweza kuchukua hatua
ziada.
Mnyika alieleza kuwa pamoja na hatua hizo za mbunge na manispaa, Rais
Kikwete naye anawajibu wa kueleza sababu za Serikali kutokutekeleza
mpaka sasa ahadi ya ujenzi wa Machinga Complex katika Jimbo la Ubungo
katika eneo la Mbezi Luis.
“Tofauti na ahadi nyingine ambazo utetezi unaweza kuwa miaka mitano ya
utekelezaji bado, suala la ujenzi wa Machinga Complex lilipaswa
kutekelezwa na kukamilika ndani ya miaka miwili kwa kuwa Rais Kikwete
wakati akihutubia hapa hapa Manzese kwenye uchaguzi wa mwaka 2010
alisema fedha za mkopo toka China zipo toka wakati huo”, alikumbusha
mbunge.
Itakumbukwa kwamba akihutubia mkutano wa kampeni tarehe 17 Oktoba 2010
kwenye eneo la Bakheresa Rais Kikwete alisema kwamba pamoja na ujenzi wa
Machinga Complex ya Jiji Ilala kutajengwa Machinga Complex nyingine
katika Manispaa zingine za Mkoa wa Dar es salaam zenye kuweza kuchukua
jumla ya wafanyabiashara ndogo ndogo 40,000.
Kwa upande mwingine, Mnyika aliwaeleza wananchi kwamba ujenzi wa
Machinga Complex pekee hauwezi kuwa ufumbuzi wa matatizo ya ajira kwa
vijana hivyo ni muhimu kuhusisha mikakati mingine yenye kuongeza
uzalishaji mijini na vijijini unaombana na ongezeko la ajira na ujira
bora.
“Tanzania haiwezi kuwa taifa la wachuuzi, tunapaswa kuwa nchi ya
wazalishaji zaidi ili kuinua uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya
wananchi. Hivyo, yanahitajika maeneo mengi ya uzalishaji sio kwa ajili
ya wakulima bali pia kwa ajili ya viwanda vidogo kwenye kutoa ajira kwa
wengi na kwa wingi”, alisisitiza Mnyika.
Mbunge alieleza kwamba ili kutekeleza azma hiyo amewawakilisha wananchi
na kuisimamia Serikali bungeni mwaka 2012 kupitia michango na maswali
kuhusu viwanda vilivyobinafsishwa au kuuzwa miaka ya nyuma katika Jimbo
la Ubungo mathalani Ubungo Garments; Ubungo Spinning Mill; Polysacks
Ltd; Tanzania Sewing Thread; Coastal Diaries (Maziwa) na Kiwanda cha
Zana za Kilimo (UFI); na hatimaye serikali ilimjibu kuwa waraka
utawasilishwa kwenye baraza la mawaziri ili kurejesha viwanda
vilivyodidimizwa kinyume cha masharti ya mikataba.
Kufuatia majibu yao mbunge alipendekeza bungeni kuwa miongoni mwa maeneo
ya viwanda yatakayorejeshwa kutengwe eneo maalum kwa ajili ya wenye
viwanda vidogo vidogo katika jimbo la Ubungo ili kupanua wigo wa ajira
hususan kwa vijana.
“Ninakwenda bungeni mwezi ujao, iwapo mpaka wakati huo Rais Kikwete
atakuwa hajaeleza sababu za ahadi ya Machinga Complex na kufuatilia
waraka huo kuhusu viwanda vilivyobinafishwa kwa kuwa yeye ndiye
mwenyekiti wa baraza la mawaziri; nitawawakilisha kwa hatua zaidi ambazo
nyinyi wananchi mtaona zinafaa”, aliahidi mbunge.
Mnyika alisema kwamba pamoja na haja ya kupata maeneo hayo ambayo vijana
wenyewe kupitia mitaji yao midogo midogo wataweza kuwekeza katika
viwanda vidogo vidogo, lipo eneo ambalo hilo Serikali inaweza kuwekeza
kwa mkopo kujenga jengo ili kuweza kutumiwa na vijana wengi zaidi katika
Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla.
“Rais akumbuke kwamba toka mwaka 2010 Serikali iliahidi kujenga jumba la
viwanda vidogo vidogo katika eneo lililokuwa mali ya TTCL Barabara la
Sam Nujoma, ni muhimu akatoa kauli kabla ya mkutano wa bunge kuanza kuwa
bilioni 100 za mkopo toka China kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la
viwanda vidogo na majengo mengine ya wafanyabiashara ndogo ndogo
zimeishia wapi?”, alihoji Mnyika.
Imetolewa tarehe 19 Machi 2013 na:
Aziz Himbuka
Katibu Msaidizi
Ofisi ya Mbunge