Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, alisema kiasi hicho cha fedha kiliwekwa kimakosa kwenye wizara ya ujenzi kwani kilipaswa kuwekwa kwenye hesabu za Wakala wa Barabara (Tanroad).
Alisema kiasi hicho kilichohojiwa na ukaguzi ni fedha ambazo zimeonyeshwa kwenye taarifa za hesabu za wizara kama vile ni miradi mipya ya mwaka 2011/2012 tofauti ni uhalisia wenyewe ulivyo.
“Uhalisia ulivyo ni kwamba fedha hizi baada ya kupokelewa na Wizara ya Ujenzi kutoka hazina zilihamishwa kwenda Tanroad, kulipia madeni ya makandarasi wa miradi ya barabara zilizotekelezwa na wakala wa Tanroad ambao walikuwa hawajalipwa mwaka wa fedha wa 2010/2011.
“Fedha hizi kimakosa zilijumuishwa kwenye hesabu za wizara kama matumizi ya akaunti ya maendeleo, hivyo kuongeza matumizi ya wizara kimakosa kwa kiasi hicho.
“Kihasibu fedha hizi zilipaswa kuonyeshwa kwenye hesabu za mtumiaji wa fedha hizi ambaye ni Tanroad, hivyo kwa sababu za wizara hazikuwa sahihi na kwa kuwa ongezeko hilo la matumizi la Sh 252,975,000 lilikuwa kubwa wizara ilipewa hati ya ukaguzi yenye mashaka,” alisema
Aidha alisema katika kujadilia hesabu za wizara hiyo, hakukuwepo na tuhuma zozote za ufisadi ila kamati ilimtaka CAG kuihakikishia matumizi ya fedha hizo jambo ambalo litafanyika.
Hivi karibuni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilisema kuwa taarifa ya matumizi ya fedha katika Wizara ya Ujenzi, ina shaka kwani kuna fedha ambazo ziliombwa kwa ajili ya miradi ambayo haipo.