Jenerali wa daraja ya juu wa Iran ameionya Marekani kwamba matokeo yanaweza kuwa mabaya iwapo Marekani itapindukia ule aliosema "mstari mwekundu" nchini Syria.
Matamshi hayo ya naibu mkuu wa jeshi la Iran, Massoud Jazayeri, yalichapishwa baada ya Rais Obama na waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, kukubaliana kwamba inafaa kujibu kwa uzito iwapo itagundulikana kuwa Syria ilitumia silaha za kemikali dhidi ya watu wake.
Syria imekanusha kuwa ilihusika na lile linalodaiwa kuwa shambulio lilofanywa Ghouta karibu na Damascus juma lilopita, ambapo silaha za kemikali zilitumiwa.