Kwa ufupi
Kama matamko ya rasimu ya Katiba Mpya na ile ya Sera
ya Elimu yatatekelezwa kwa ufanisi, bila shaka elimu nchini itapiga
hatua kubwa siku zijazoHAKILEO
Hivi sasa elimu ya Tanzania inasimamiwa na
kuongozwa na Sera ya Elimu ya mwaka 1995, ambayo wadau wa elimu wanasema
kuwa imepitwa na wakati.
Mbali na sera hiyo, Katiba ya nchi kama sheria
mama pia ina mkono wake katika kusimamia elimu. Kwa sasa katiba yenye
jukumu hilo ni ile ya mwaka 1977 ambayo bado inatumika kuliongoza Taifa
letu.
Leo kila Mtanzania anayefuatilia mambo, anatambua
kuwepo kwa Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
ile ya Sera ya Elimu na Mafunzo, ambazo zote zipo kwenye hatua ya
kutolewa maoni na wadau.
Ikumbukwe kuwa, kutokana na Sera ya Elimu iliyopo
ambayo inasema kuwa elimu ya lazima ni ile ya darasa la saba, watoto
wengi wanakosa fursa ya elimu ya sekondari kutokana na wazazi au walezi
kuwakatisha masomo na kuwalazimisha kuolewa ama kufanya shughuli
nyingine.
Bila shaka mustakabali wa elimu yetu kwa miaka
mingi ijayo, unategemea kwa kiwango kikubwa kile kitakachopitishwa
kwenye Katiba mpya ijayo pamoja na sera mpya ya elimu.
Katiba Mpya
Kwa mfano, katika rasimu eneo la haki ya elimu na
kujifunza ibara ya 41, -(1) inasema kila mtu ana haki ya kupata fursa ya
kupata elimu bila ya vikwazo, kupata elimu bora ya msingi bila ya
malipo na inayomtayarisha kikamilifu mwanafunzi, ama kuendelea na elimu
ya ngazi inayofuatia au kuweka msingi wa kuanza kujitegemea.
Kwa elimu inayotolewa nje ya utaratibu wa umma,
itolewe kwa gharama nafuu na pia kuwepo fursa sawa ya mtu kupata elimu
ya juu, ilimradi ana sifa stahiki ya kupata elimu hiyo bila ya ubaguzi
wa aina yoyote.
Kwa madhumuni ya Ibara ndogo ya (1), kila mtu ana
haki ya kuchagua taaluma na ajira anayoitaka kwa mujibu wa elimu yake na
ujuzi aliyonao,” inasema sehemu hiyo ya Rasimu ya Katiba.
Mbali na ibara hiyo, haki ya elimu imeguswa tena
kwenye eneo la Haki ya Mtoto katika ibara ya 42. Ibara hiyo inasema kila
mtoto ana haki ya kucheza na kupata elimu.
Hivi ndivyo rasimu ya Katiba Mpya inavyosema
kuhusu suala la elimu kwa wananchi ikisisitiza kuwepo kwa elimu bora ya
msingi kwa kila mtoto itakayotolewa bila ya malipo na inayomtayarisha
kikamilifu mwanafunzi ama kuendelea na elimu ya ngazi inayofuatia au
kuweka msingi wa kuanza kujitegemea.