Rais wa Zimbabwe, Robert MugabeDALILI za ushindi wa kiti cha urais kwa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe dhidi ya mpinzani wake, Morgan Tsvangirai, zinamuweka kiongozi huyo kwenye kundi la viongozi ambalo nchi za Magharibi zimeshindwa kuwaondoa madarakani, kwa kutumia sanduku la kura au migongo ya wapinzani wao.
Mwelekeo huo wa ushindi wa Rais Mugabe, unafanana na ule wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, ambaye alishinda uchaguzi kwa nguvu ya sanduku la kura, licha ya Mataifa ya Magharibi kudaiwa kujaribu kutumia kila aina ya njia kuuzuia ushindi wake.
Mpinzani wa Uhuru, Raila Odinga, aliyetajwa kupigiwa chapuo na nchi za Magharibi, alishindwa kuchukua nafasi ya ukuu wa dola katika uchaguzi wa Machi mwaka huu, baada ya kuangushwa kwenye sanduku la kura.
Kama ilivyo kwa Mugabe, ambaye anaongoza Chama cha ZANU-PF, Mpinzani wake, Morgan Tsvangirai wa Chama cha Movement for Democratic Change (MDC), naye amekuwa akitajwa kama pandikizi la nchi za Magharibi, lakini pamoja na sapoti ambayo amekuwa akidaiwa kupatiwa, hata hivyo anaonekana kushindwa kuteka mioyo ya Wazimbabwe.
Tofauti na Uhuru Kenyatta, ambaye kwa mara ya kwanza amekuwa Rais wa Kenya, Mugabe yeye tayari ametawala Zimbabwe kwa takribani miaka 33 na hivyo kutajwa kama muasi wa demokrasia.
Matarajio ya watu wengi nje ya mipaka ya Zimbabwe yamekuwa ni tofauti katika uchaguzi wa mwaka huu, kwa sababu Tsvangirai ndiye aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ukilinganisha na Mugabe.
Hii inatokana na nguvu aliyoionyesha Tsvangirai katika uchaguzi wa mwaka 2008, ambapo alionekana kumtikisa Mugabe, ambaye hata hivyo alimzidi kwa kura.
Pigo la kwanza kwa Tsvangirai na watu wanaodaiwa kuwa nyuma yake ni ushindi wa sasa wa Chama cha Rais Mugabe cha ZANU-PF, kwenye viti vya ubunge.
Kwa mujibu wa matokeo ya Tume ya uchaguzi ya Zimbabwe, yanaonyesha kuwa katika viti 210 vya ubunge, chama cha Zanu-PF kimeshinda viti 137 kati ya 186 ambavyo matokeo yake tayari yamekwisha hesabiwa.
Kwa matokeo haya, ni wazi kwamba, Wazimbabwe wengi, licha ya kupita kwenye kipindi kigumu cha matatizo ya kiuchumi baada ya kuwekewa vikwazo na nchi za Magharibi ambavyo vilisababisha nchi kukumbwa na mfumuko mkubwa wa bei, Mugabe bado anaonekana kuwa ni mwenzao, tofauti na Tsvangirai ambaye wengi wanaamini kuwa ni pandikizi la Magharibi.
Pigo lingine kubwa ni kitendo cha Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kile cha Mkuu wa Waangalizi wa Uchaguzi kutoka AU, Rais wa Zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, kusema kuwa uchaguzi huo umekuwa huru na amani na kupuuzia malalamiko ya udanganyifu.
SADC, katika taarifa yake, licha ya kusema kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa amani, ilikwepa kusema kama ulikuwa wa haki kwa kile walichodai kuwa bado mapema kusema hivyo.
Hata hivyo MDC tayari wametamka bayana kwamba hawatatambua matokeo hayo, kwa madai ya kuwapo kwa udanganyifu.
Chama hicho tayari kimeitisha mkutano wa dharura kwa ajili ya kujadili matokeo hayo.
Ingawa matokeo ya kura za urais bado hayajatangazwa, kutokana na mabadiliko ya Katiba ya nchi hiyo, mshindi ni lazima apate asilimia 50 ya kura zilizopigwa