- www.hakileo.blogspot.comALIKUWA NA WENZAKE WAPORA DOLA 20,000
Na Masau
Bwire
JESHI la Polisi Mkoa wa Ilala,
linawashikilia watu wanne akiwemo
askari wake mmoja kwa tuhuma za kufanya ujambazi kwa kutumia silaha (bastola)
na kupora dola za Marekani 20,000, sawa na sh. milioni 32 za Tanzania.
Askari
huyo amefahamika kwa jina la Mohamed Mhina ambaye kituo chake cha kazi ni
Oysterbay, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ambaye akiwa na wenzake wanne,
walikwenda kufanya uhalifu nyumbani kwa mkazi mmoja wa eneo la Klabu ya
Wazee,iliyopo Bungoni, Ilala, Dar es Salaam.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili, umebaini askari huyo alihamishiwa kituoni hapo
akitokea Kituo cha Polisi Kimara,ambapo katika uhamisho wake alikuwa bado
hajaanza kuutekeleza kwa sababu alikuwa likizo.Tukio
hilo limetokea usiku wa kuamkia jana baada ya askari huyo na mwenzake, kupata
taarifa kuwa kuna mtu ambaye si raia wa Tanzania aliyekuwa na fedha; hivyo
walikwenda kumvamia nyumbani kwake ili wazichukue.
Watuhumiwa
hao walifanikiwa kuingia nyumbani kwa mtu huyo, kumtaka awape fedha alizonazo
na kupewa dola za Marekani 20,000 baada ya kumtisha kwa bastola.Wakati
wakijiandaa kutoka nje ya nyumba hiyo, rafiki za mtu aliyevamiwa na kuporwa
fedha hizo walifungua geti, kuingia ndani na kukuta hali tofauti; hivyo baada
ya kuuliza kuna nini, aliyeporwa fedha hizo baada ya kusikia sauti za rafiki
zake aliitika kwa sauti “nimevamiwa na majambazi”.
Wakati huo, askari
huyo na wenzake walijificha nje ya nyumba hiyo na baada ya kusikia sauti hiyo,
aliyekuwa na fedha hizo ambaye pia ndiye aliyekuwa ameshika bastola, aliruka
ukuta na kutokomea kusikojulikana akiwaacha wenzake.Rafiki wa mtu
aliyeporwa fedha hizo, walipambana na askari huyo pamoja na wenzake watatu
ambao walichelewa kuruka ukuta na kufanikiwa kuwakamata.
Watuhumiwa hao
wamefikishwa katika Kituo cha Polisi Msimbazi ambapo Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Ilala, Marietha Minangi, alithibitisha kukamatwa kwa askari huyo na kusema
taarifa zaidi juu ya tukio hilo atazitoa leo.Naye Kamanda wa Mkoa
wa Kipolisi Kinondoni, Camilus Wambura, amekiri kuwa askari huyo alihamishiwa
kituoni kwake, lakini amekamatwa kwa ujambazi.
Majina ya watuhumiwa wengine pamoja na nile la mtu aliyeporwa fedha hizo, hayakuweza kufahamika mara moja.Taarifa za uhakika kutoka kwa baadhi ya askari, zinasema mama mzazi wa askari huyo anafanya kazi ofisi moja na kigogo wa jeshi hilo Makao Makuu ya Polisi.