AIBU,Meli ya Tanzania yanaswa na tani 30 za bangi Italia

HABARI ZETU


Meli ya Gold Star iiliyosajiliwa Tanzania ikiwaka moto baada ya mabaharia wake kuichoma iliponaswa ikiwa imebeba dawa za kulevya aina ya bangi katika pwani ya Italia juzi. Picha ya Reuters  
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi KWA MUJIBU WA GAZETI LA MWANANCHI.
KWA UFUPI
  • Imesajiliwa Zanzibar na wakala wa Dubai, mzigo una thamani ya Sh125 bilioni, mabaharia wajaribu kuichoma moto, wajitosa baharini

Zanzibar.
 Jina la Tanzania limechafuliwa tena baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa ikiwa na tani 30 za dawa za kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Pauni za Uingereza 50 milioni (Sh125 bilioni).
Tukio hilo limetokea miezi miwili baada ya Watanzania wawili kukamatwa na dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 na thamani ya Sh6 bilioni kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini.
Habari zilizothibitishwa jana na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA), Abdi Omar zilisema kwamba meli hiyo ilikamatwa juzi ikiwa na mzigo huo wa bangi.
Alisema baada ya kupokea taarifa za kukamatwa kwa meli hiyo kutoka kwa Polisi wa Kimataifa (Interpol), ofisi yake iliwasiliana na wakala wake aliye na ofisi zake Dubai, Falme za Kiarabu, Kampuni ya Philtex ambayo alisema inafanya kazi ya kusajili meli kwa niaba ya Serikali na kuthibitisha kuisajili.
Alisema meli hiyo ilisajiliwa mwaka 2011 kwa kazi ya kubeba mizigo chini ya Kampuni ya Gold Star.
Alisema kutokana na tukio hilo, Kampuni ya Gold Star imekiuka masharti ya Sheria ya Usajili wa Meli na ile ya Umoja wa Mataifa zinazozuia meli kubeba dawa za kulevya na kuongeza kwamba ofisi yake itafanya uchunguzi na kuchukua hatua.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema naye amesikia kupitia kwenye mitandao kwamba hajapata taarifa za kina... “Leo ni Jumapili ni ngumu pia kupata taarifa rasmi kuhusiana na hili.”
“Kesho (leo) tutawasiliana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) ili kufahamu undani wa suala hili. Kuanzia hapo ndipo tutajua nini kinachoendelea, kama waliokamatwa ni Watanzania au la na hiyo bangi waliitoa wapi.”
Msemaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), David Mziray alisema: “Sina taarifa za tukio hilo, labda tuwasiliane kesho.”
Kama sinema
Taarifa zilizopatikana jana kwenye mitandao mbalimbali ya kimataifa zinasema meli hiyo ilinaswa maofisa Forodha na askari wa doria wa Italia waliokuwa Pwani ya Sicily, Bahari ya Mediterania.
Msemaji wa Idara ya Ushuru Italia, alisema: “Meli hiyo ilikamatwa baada ya kupatikana kwa taarifa za kiitelijensia kuwa imebeba dawa hizo, lakini hatukutarajia kama kungekuwa na mzigo mkubwa kiasi hicho na hata wahusika kuipiga moto
Taarifa hizo zilisema helikopta na boti za kasi za polisi zilianza kuisaka meli hiyo na kwamba kitendo cha mabaharia hao kuichoma, moto kiliwafanya kubaini kilichokuwamo kutokana na harufu kali iliyokuwa ikitoka.
Msemaji huyo alisema Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji wa Bahari Italia kiliitwa kuuzima... “Walikuwa wakijaribu kuharibu ushahidi ili wasionekane na makosa ya kujibu lakini mpango wao ukafeli, moto ukawa unarusha bangi hiyo na zaidi iligundulika baada ya kuikagua.”
Mbali na kuzima moto huo, kazi nyingine ilikuwa kuwaokoa mabaharia hao tisa ambao maofisa wa Italia walisema ni raia wa Syria na Misri.
“Walijirusha kutoka melini na walikuwa mbali sana na kilichofanyika ni maofisa wa forodha kuwafuata na kuwasaidia,” alisema.
Meli hiyo iliyotengenezwa miaka 38 iliyopita, inashikiliwa kwenye Bandari ya Syracuse na manahodha wake wamekamatwa na wanahojiwa na polisiwww.hakileo.blogspot.com
.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company