
Katika hali isiyotarajiwa hapo jana bodi ya wadhamini wa kanisa la Tanzania Assemblies of God nchini jijini Mwanza iliamua kwenda mahakamani kuwasilisha pingamizi la kutoruhusu mwili wa aliyekuwa askofu mkuu wa kanisa la E.A.G.T marehemu Dkt. Moses Kulola kuzikwa katika viwanja vya kanisa hilo lililopo maeneo ya Bugando jijini Mwanza wakidai ni mali yao jambo ambalo hata hivyo haikuwezekana na mwili huo utazikwa kama ilivyopangwa mapema hii leo.
Akizungumza na WAPO Radio Fm kupitia kipindi cha habari Yaliyotokea askofu Lameck Mkumba wa E.A.G.T amesema ameshangazwa na uamuzi huo kwakuwa waumini wa kanisa la E.A.G.T wamekuwa wakilitumia kanisa hilo la Bugando kwa muda mrefu sasa bila kuwapo matatizo yeyote hadi kuibuka kwa suala hili ambalo hawakutarajia" Mimi mwenyewe nina miaka zaidi ya 15 nikiwa muumini na niliokoka ndani ya kanisa hili la Bugando E.A.G.T" amesema askofu Mkumba
Aidha askofu huyo amesema baada ya kuona wenzao wametumia taratibu za kisheria kwakutumia bodi ya wadhamini wao mahakamani ikabidi nao pia kutafuta uwakilishi wa kisheria ambao uliwasimamia vyema kwakuwasilisha vielelezo na maelezo ya msingi ambayo mahakama iliridhika nayo nakuamua kuwapa kibali cha kuendelea na maziko ya askofu Kulola katika viwanja hivyo.

Wakati huo huo askofu mkuu wa kanisa la T.A.G Barnabas Mtokambali anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari ofisini kwake saa nne asubuhi leo kwaajili ya kutolea ufafanuzi baadhi ya mambo baada ya kuulizwa na mtangazaji wa WAPO Radio FM Beatrice Kamanga kupitia kipindi cha Yaliyotokea akitaka kujua amepokeaje hali iliyojitokeza huko Mwanza hapo jana.
![]() |
Hapa ndipo atakapolala Askofu MKuu Moses Kulola |