MSIBA;NAHODHA, MAOFISA JWTZ WAMUAGA MLIMA



Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha jana aliwaongoza maofisa wa JWTZ katika kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Luteni Rajab Ahmed Mlima.

Marehemu Luteni Mlima, aliuawa akiwa katika Uwanja wa Mapambano na wanagambo wa Kundi la Waasi wa M23, katika Milima ya Gavana, karibu na Goma, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakati akitekeleza jukumu la ulinzi wa amani.

Viongozi wengine walioshiriki katika kutoa heshima zao za mwisho kwa ofisa huyo, ni pamoja na waziri wa zamani katika wizara hiyo Profesa Philemon Sarungi, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Luteni Jenerali Samuel Albert Ndomba na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoa heshima hizo, Waziri Nahodha alisema Serikali inatoa pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange, kwa kumpoteza mtu shujaa aliyekuwa akitetea roho za watu.

Alisema hata hivyo, Serikali haitarudi nyuma katika masuala ya ulinzi wa amani, na kwamba itaendelea kutoa msaada wa ulinzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hadi hapo amani itakapopatikana.

"Kwa kweli tumepata pigo kubwa la kuondokewa na shujaa wetu, lakini sisi kama Serikali hatutarudi nyuma kwenye masuala ya ulinzi wa amani hadi pale tutakapoona amani imepatikana,"alisema Nahodha.

Waziri huyo alisisitiza kwamba Serikali itaendelea kutoa msaada kwa familia ya marehemu Luteni Mlima, kwani hilo ni jukumu lake.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Luteni Jenerali Ndomba, alisema Luteni Mlima amefariki kishujaa wakati akilinda amani na kwamba siku zote jeshi litatambu mchango wake.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company