Waasi nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo watakiwa kujisalimisha


Wanajeshi wa DRC wakiwa mjini Bunagana

Na Victor Melkizedeck Abuso
Jeshi la Umoja wa Mataifa MONUSCO linalolinda amani huko nchini Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo limetoa wito kwa makundi ya waasi kujisalimisha wakati ambapo jeshi la FRDC limefanikiwa kudhibiti maeneo yaliyokuwa yakikaliwa na waasi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Abdalah Wafi amesema makundi yote ya waasi yajisalimishe kwa jeshi la Congo na kuwatoa hofu zaidi kwa wanaoshindwa kujisalimisha kwa jeshi wasisite kufanya hivyo katika ofisi za makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Aidha Ujumbe wa EU uliarifu kuwa wakati umefika kwa suluhu la kisiasa kupatikana kati ya serikali ya DRC na waasi hao jijini Kampala ili kurejesha amani Mashariki mwa nchi hiyo.

Umoja huo unasema kuwa ni muhimu sana kwa mazungumzo hayo pia kutumiwa kumaliza makundi mengine ya waasi Mashariki mwa nchi hiyo.

Kauli hiyo ya EU inakuja wakati Jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo likiendelea kupambana na waasi wa M 23 baada ya kudhibiti ngome yao ya mwisho katika mji wa Bunagana karibu na mpaka wa Uganda.

Wakaazi wa mji huo walisema kuwa walisikia mapambano usiku kucha huku mkaazi mmoja akiliambia Shirika la Habari la Ufaransa la AFP kuwa msichana mmoja alijeruhiwa kwa kupigwa risasi wakati wa makabiliano hayo.

Wakati mapambano hayo yakiendelea, Marekani imetoa wito kwa waasi wa M 23 na Serikali ya Kinsasha kurudi katika meza ya mazungumzo ili kupata suluhu ya kudumu kuhusu hali ya Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Jeshi la Serikali linasema kuwa lilianzisha oparesheni hiyo ili kuhakikisha kuwa waasi hao wanaondoka kabisa katika mji huo ambao umekuwa kama makao yao makuu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Siku ya Alhamisi, Msemaji wa serikali ya DRC Lambert Mende alisema kuwa jeshi la serikali lilifanikiwa kuchukua mji wa Bunagana na kuongeza kuwa nafasi ya mazungumzo ya amani jijini Kampala ilikuwa wazi.

Ripoti zinasema kuwa, waasi wa M 23 waliokuwa wanapiga kambi katika ngome yao ya kijeshi ya Bunagana wanaelezwa kutorokea kusikojulikana huku kiongozi wa kundi hilo Betrand Bissimwa akiripotiwa kukimbilia nchini Uganda.

Serikali ya Uganda imethibitisha kuwa Bissimwa yuko nchini humo baada ya kuitwa na msuluhishi Mkuu wa mazungumzo ya amani kati yao na serikali ya DRC Crispus Kiyonga.

Mwakilishi wa serikali ya Kinsasha katika mazungumzo hayo ya amani Francois Muamba, amedokeza kuwa ikiwa kundi la M 23 litakubali mapendekezo waliyotoa basi kuna matumaini kuwa suluhu likapatikana haraka.

Mapema juma hili mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa MONUSCO katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Martin Kobler aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa kundi la waasi la M 23 sio tishio tena kijeshi Mashariki mwa nchi hiyo.

Mapigano kati ya waasi na majeshi ya serikali yalianza wiki iliyopita baada ya mazungumzo ya amani kuvunjika jijini Kampala Uganda na kufikia siku ya Jumatatu jeshi la serikali lilifanikiwa kuchukua miji ya Rutshuru, Kiwanja na Rumangambo yote ambayo hapo awali ilikuwa inadhibitiwa na waasi hao kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company