Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Mvomero, Amos Makala akizungumza katika mkutano wa wakulima na wafugaji uliofanyika katika Kijiji cha Mkindo wilayani Mvomero. Kutoka kulia ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chizza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dk Mathayo David, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Gudluck Ole-Medeye. Picha na Elias Msuya.
Mvomero.Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala juzi aliwekwa kitimoto na baadhi ya wakulima wilayani Mvomero mbele ya mawaziri wengine wanne katika mkutano ulioitishwa kutafuta suluhu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Mkindo.


Makala ambaye pia ni Mbunge wa Mvomero ulipo mgogoro huo, alilalamikiwa na wakulima hao wakidai kwamba amekuwa akiwasikiliza zaidi wafugaji na kutoonyesha
jitihada za kumaliza tatizo hilo.
Mawaziri wengine waliohudhuria mkutano huo kwa agizo la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chizza, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Gudluck Ole-Medeye.


Akijibu shutuma zilizoelekezwa kwake, Makala alisema: “Msiseme tu mwangalie na juhudi zangu. Namshukuru Dk Nchimbi kwa kusoma barua ya Waziri Mkuu, uongo umejitenga na ukweli umedhihirika. Mimi nikiwa mbunge ni mwakilishi wa wananchi, nimewaita mawaziri hapa, nimekuwa kama mshenga ili wasikie malalamiko yenu,” alisema Makala.


Malalamiko ya wananchi


Katika malalamiko yao, wakulima hao walisema licha ya uonevu wanaoupata kutoka kwa wafugaji na Jeshi la Polisi, mbunge wao amekuwa kimya.


“Mbunge wetu hatusaidii kitu kila tunapopata matatizo. Yalipotokea machafuko Kijiji cha Hembeti hakuonekana. Kuna taarifa zisizo rasmi kuwa amekuwa akifanya mapatano na wafugaji kwa siri,” alisema mmoja wa wanakijiji wa Mkindo, Shomari Msumi na kuongeza:


“Watoto wetu wamelazwa Hospitali ya Bwagala, Polisi wamekuja kuwafunga pingu na kuondoka nao, wafugaji hawaguswi kwa sababu ya nguvu ya fedha. Vyombo vya Dola hasa Mahakama nayo inatukwamisha. Mazao yameliwa lakini kesi haziamuliwi, hadi leo kesi iko wilayani.”


Mkulima mwingine, Aziz Dendego alisema: “Tunaumizwa mno na viongozi wa wilaya. Mimi nimefika hapa mwaka 1975. Kero zimeanza miaka 20 iliyopita na Serikali ndiyo inayosababisha. Mkuu wa Mkoa anaagiza tu lakini hatuoni vitendo. Mkuu wa wilaya alikuwa mzuri lakini sasa amebadilika kabisa. Bunduki za kijeshi zimetumika kwenye mapigano, wakulima wamezipataje?”


Mmoja wa wakulima hao, Shaaban Khamis alisema wameamua kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi baada ya kulalamika kwa muda mrefu bila kusikilizwa.


Wakulima hao pia wamemlalamikia Mwenyekiti wa Kijiji cha Wafugaji cha Kambala waliyemtaja kwa jina moja la Kashu wakidai kuwa amekuwa akiongoza mapigano dhidi ya wakulima.Hata hivyo, Kashu hakuhudhuria mkutano huo ambao wafugaji waliwakilishwa na mfugaji mmoja tu, Majuka Koila.


“Watu wameuawa, nyumba 380 zimechomwa moto na wafugaji katika Kijiji cha Kwa Mbogo, hadi leo hakuna aliyekamatwa,” alisema Hassan Said.


Mawaziri wamtetea


Licha ya Dk Mathayo kuahidi kujenga majosho na mabwawa ya kunyweshea mifugo, alimtetea Makala kuwa amekuwa akimsumbua kuhusu matatizo ya wakulima.


“Makala anakaa nyuma yangu pale bungeni, amekuwa akinisumbua sana. Mbunge wenu anawapenda,” alisema na kuongeza:


“Lazima wafugaji wafuate sheria na utaratibu. Matatizo haya yanatokana na ukosefu wa miundombinu hasa malambo na majosho. Tutayajenga ili wafugaji wasiingie kwa wakulima.”


Huku akimtetea Makala, Naibu Waziri, Ole-Medeye alitaja mikakati mitatu ya Serikali.


“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Shetani kazi yake ni kusababisha vita na ugomvi kati ya ndugu na ndugu. Makala amenisumbua sana. Migogoro mingi imekuwapo kabla hata hajaingia madarakani. Kwa mfano, mgogoro huu wa Bonde la Mgongola umeanza mwaka 2005, Makala alikuwepo?”


Kuhusu utatuzi wa mgogoro huo, Ole Medeye alisema amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kumaliza suala hilo nje ya mahakama ili kuleta suluhu.


Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka alipojaribu kumtetea kwa kuwauliza wananchi kama Waziri Makala ameshawatembelea mara ngapi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkindo, Ally Shamte alisema amefika mara moja tu tangu achaguliwe.


Waziri Chizza alikiri kuwa kero za wakulima zinatokana na kutopewa majibu haraka... “Lipo tatizo la kutotoa majibu haraka. Tunao mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), tunapaswa kutoa majibu sasa siyo kusubiri matukio. Tusingependa kuja hapa baada ya watu kufa, maana hatuwezi kuwafufua,” alisema Chizza.Baada ya mawaziri hao kujieleza, Chizza alimpa nafasi Makala ambaye alieleza kwa kina jinsi alivyoshughulikia migogoro hiyo.


“Ulipotokea mgogoro wa Kijiji cha Lukenge, nilikaa na wafugaji wa Kijiji cha wafugaji cha Sokoine na siku hiyohiyo nilikaa na wakulima wa Kijiji cha Sigaju. Siku walipofunga barabara nilikuwa mkoani Iringa kwenye sherehe za kuzima Mwenge. Watu wanafanya siasa, wengine wananipigia simu na kuniuliza niko kijijini, hayo ni mambo ya siasa tu,” alisema na kuongeza:


“Mgogoro wa Bonde la Mgongola tumekuja pale wakatoa tamko, shamba la Kijiji cha Begi hakuna mwanasiasa yeyote aliyeshughulikia zaidi yangu. Nimekaa pale hadi saa mbili usiku. Hata wale vijana waliosingiziwa kesi nimetoa fedha yangu mfukoni kuwatoa.”


Dk Nchimbi awajia juu polisi


Licha ya kumtetea Makala, Dk Nchimbi alishangazwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kutowakamata wafugaji waliohusika katika mapigano hayo.


“Binafsi sijaridhishwa na idadi ya wafugaji waliokamatwa. Haiwezekani wauawe watu sita, wakulima wanne na wafugaji wawili halafu wakamatwe wakulima 32 na wafugaji wawili. Hakikisha unafanya operesheni ya kuwakamata waliohusika,” alisema Dk Nchimbi.


Awali, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alikanusha kuwa bunduki zilizotumika kwenye mapigano hayo zilikuwa za kijeshi.


“Baada ya tukio, maganda yaliyookotwa yalikuwa ya bunduki za aina ya ‘shot gun na rifle’. Hata yule mfugaji aliyeuawa bunduki yake imesalimishwa siyo ya kijeshi,” alisema.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company