Ni upepo tu utapita, ndiyo msemo unaotawala sasa hivi hata kwenye masuala ya msingi yanayogusa mustakbali wa Taifa.
Kwa kuwa watawala wameanzisha huo msemo kwa vitendo basi hata wananchi nao wameanza kuutumia, hata kwa mambo ambayo watawala wanapanga kuyafanya kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Hata ungekuwa wewe ungestaajabu pale unapomuuliza Mwalimu Mkuu wa shule fulani kuwa unaufahamu “Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa”? akakujibu: “Nausikia tu ila huo ni upepo tu”. Muulize swali la pili, kwa sababu gani anasema ni upepo? Anajibu kwa muundo wa swali: “Iko wapi ripoti ya Tume ya Waziri Pinda ambayo wajumbe walilipwa fedha nyingi za walipa kodi?”
Endelea na swali la tatu: Ni Ripoti ya Tume ya Pinda tu ndiyo inakufanya useme ni upepo? Anajibu, “Hadi leo siujui mtalaa wa elimu una sura gani licha ya kuwa ulikuwa kaa la moto katika Bunge la mwezi Februari. Ndiyo maana nakuambia kila hoja au mjadala kwa sasa ni upepo tu kwa Serikali yetu”
Jibu hili linanikumbusha mbali, kwani hata mimi sitausahau mwezi Februari 2013 kwa sababu ni kipindi kilichokaribia kutupa majibu ya kwa nini elimu yetu inashuka.
Mwezi huo ulitawaliwa na mjadala kuhusu mtalaa wa elimu, Sera ya Elimu na ubovu wa vitabu vya kiada vinavyotumika shuleni. Bunge lilithubutu angalau kutaka kupata majibu, lakini kwa mshangao wa wengi, mjadala ulipotea kimya kimya bila Watanzania kupata majibu sahihi.
Japo miezi minane imepita, nilidhani tungepata majibu ya kuwa na mtalaa wa elimu kisha ukasambazwa shuleni na kila mwalimu, lakini hadi leo hii hatima ya mtalaa imebaki siri kubwa ya watawala.
Hivi karibuni wamejaribu kuweka kitu kama rasimu ya mtalaa kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, eti wanaiita mitalaa na wanakaribisha maoni kwa Kamishna wa Elimu.
Hivi kweli viongozi hawa wako makini? Je, ni kweli huu ulikuwa upepo tu na sasa umeshapita kama wasemavyo watawala na wananchi. Binafsi bado siamini kama ule mtalaa uliopitiwa na kamati maalumu ya Bunge ulikuwa mtalaa sahihi.
Aidha, hata nikiamini kuwa ulikuwa sahihi, napata swali jingine tena, “Hivi hadi leo Serikali imeshindwa japo kutoa nakala nyingine na kuzipeleka kwenye shule au hata kuweka kwenye tovuti ya wizara husika?”
Mjadala wa ubovu wa vitabu ulimgusa kila Mtanzania, na nilidhani hili lingekuwa fundisho kwa watawala kubaini makosa ya vitabu hivi na hatimaye kuwa na vitabu stahili.
Hadi sasa vitabu hivi bado vinatumika shuleni na pia Serikali imeongeza vitabu vya aina ile ile kwa kutumia chenji ya Rada! Ama kweli na huu ulikuwa upepo tu na wala mbunge James Mbatia asingeweza kufua dafu kwa watawala. Naamini hata yule mwalimu hakukosea kusema kila hoja ya msingi ni upepo tu.
Katika mijadala hii, Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, nayo ilikuwa sehemu ya mjadala na nilidhani Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ingeukamilisha kwa kuwapatia Watanzania sera mpya.
Nakumbuka mapitio ya sera hii yalianza mwaka 2008, lakini hadi leo hatujapata sera mpya. Licha ya Rais Jakaya Kikwete kutoa ahadi kule Mbeya wakati wa Sherehe za Mei Mosi kuwa sera mpya iko mbioni kutoka, nadhani nao ulikuwa upepo tu kwani Wizara imeendelea kuwa bubu kuzungumzia ni lini sera hii itaanza kutumika.
Godfrey Boniventura ni Meneja Idara ya Uchambuzi wa Sera na Utafiti-HakiElimu; Anapatikana kwa barua pepe; media @ hakielimu.org
www.hakileo.blogspot.com