Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC, Josephu Kabila akisikiliza jambo kwenye moja ya vikao vya nchi za maziwa makuu uliofanyika mjini Kampala mwezi September mwaka huu
Reuters
Na
Emmanuel Richard MakundiSerikali ya jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na waasi wa kundi la M23 hii leo wanatarajiwa kutia saini mkataba wa amani kumaliza machafuko mashariki mwa nchi hiyo yaliyodumu kwa miongo kadhaa.
Shughuli ya utiwaji saini inatarajiwa kufanyika mjini Kampala Uganda ambako mazungumzo ya amani yamekuwa yakifanika kujaribu kuzipatanisha pande hizo mbili kumaliza machafuko ya mashariki mwa nchi hiyo.
Utiwaji saini huo unafanyika wakati huu ambapo jeshi la Serikali la FARDC likisaidiwa na vikosi maalumu vya Umoja wa Mataifa UN vilivyoko nchini humo wakifanikiwa kuwasambaratisha wapifganaji hao kwenye maeneo ambayo walikuwa wanayakalia kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu.
Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa iwapo makubaliano hayo ya amani yatatiwa saini kutashuhudiwa kumalizika kwa miongo kadhaa ya vita kwenye eneo hilo la nchi za maziwa makuu ambapo mamia ya wananchi wamepoteza maisha na wengine kukimbia makazi yao.
Hata hivyo haijajulikana iwapo Serikali ya Kinshasa itatia saini mkataba wa amani ama azimio la kusitisha vita kati yake na waasi wa M23 kama msemaji wa Serikali hiyo Lambert Mende alivyonukuliwa mwishoni mwa juma lililopita akisema watakachotia saini ni azimio la kusitisha vita na sio mkataba wa amani.
Tayari viongozi kadhaa wa kundi la M23 wamewasili mjini Kampala huku wengine wakiendelea kuwa mafichoni na baadhi yao wakishikiliwa na majeshi ya Uganda baada ya kukimbia mapigano juma moja lililopita.
Serikali ya Uganda imesema haitawakabidhi viongozi wa kundi hilo wala wapiganaji wao endapo Serikali ya Kinshasa haitatia saini mkataba wa amani kati yake na kundi hilo jambo ambalo tayari limezua hali ya sintofahamu.
Kundi la waasi wa M23 juma moja lililopita lilitangaza kuweka silaha chini na kuacha uasi mashariki mwa nchi hiyo baada ya kuzidiwa nguvu na vikosi vya Serikali na vile vya Umoja wa Mataifa.
Nchi za Rwanda na Uganda zimejikuta zikitengwa na jumuiya ya Kimataifa kwenye baadhi ya mambo kutokana na madai kuwa zimekuwa zikiwasaidia waasi wa M23 kwa zana za kijeshi na mafunzo, tuhuma ambazo nchi hizo mbili zinakanusha.