Kamishna wa Kaunti ya Garissa nchini Kenya amesema kuwa, watu sita wameuawa baada ya kundi la al Shabab la Somalia kushambulia eneo la Liboi, lililoko katika mpaka wa nchi hizo mbili.
Kamishna wa Kaunti ya Garissa Rashid Khator amesema kuwa, askari polisi wanne na raia wawili wameuawa kwenye shambulio hilo, lililojiri umbali wa kilomita 15 kutoka mpaka wa Kenya na Somalia. Kamishna Rashid Khator amesema kuwa, wanamgambo wawili wa al Shabab nao waliuawa kwenye shambulio hilo. Kundi la al Shabab limetekeleza mashambuilio kadhaa dhidi ya vikosi vya usalama na raia wa nchini Kenya.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, mwezi Septemba mwaka huu, kundi la al Shabab lilitekeleza shambulio kwenye jengo la maduka ya biashara la Westgate mjini Nairobi na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 67. Kundi la al Shabab lilifanya shambulio hilo kwa lengo la kuishinikiza serikali ya Kenya kuondoa majeshi yake nchini Somalia. Majeshi ya Kenya yako nchini Somalia chini ya mwamvuli wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika.