Kamati ya tume ya uchaguzi iliyotangaza matokeo ya kura ya maoni kuhusu katiba mpya
Mamlaka nchini Misri imetangaza kuwa katiba mpya ya taifa hilo imeungwa mkono na 98.1% ya watu waliopiga kura katika shughuli ya kura ya maamuzi wiki jana.
Serikali hiyo inayoungwa mkono na jeshi,imesema kuwa hatua hiyo ni mwanzo mpya wa taifa la Misri.
Lakini vuguvugu la Muslim Brotherhood lililosusia kura hiyo limesema kuwa,asilimia 40 ya watu ambao hawakuinga mkono inaonyesha wazi kwamba shughuli hiyo ilifeli.
Katiba hiyo itachukua mahala pa sheria zilizowekwa na aliyekuwa rais wa taifa hilo Mohammed Morsi ambaye aliondolewa madarakani mwaka uliopita.
Waziri wa maswala ya kigeni nchini marekani John Kerry ,amesema kuwa demokrasia ni kuwepo kwa zaidi ya kura moja ,huku akitoa wito kwa serikali kuidhinisha haki na uhuru ambao katiba hiyo inapigania.
Idadi ya waliojitokeza ilikuwa 38.6% ya watu milioni 53 wenye kadi za kupiga kura.
Kura ya maoni kuhusu katiba mpya ni hatua ya serikali kutaka kuhalalisha hatua ya kumwondoa mamlakani Morsi mwaka jana.
Watu kadhaa walifariki kwenye ghasia zilizotokea wakati kura ya maoni ilipokuwa inafanyika.