Sehemu ya Barabara ya Mlandizi- Chalinze, ikiwa imeharibika kutokana magari makubwa kuzidisha uzito na kusababisha uharibifu huo.Picha na Maktaba
Na Elias Msuya,
MwananchiDar es Salaam: Uamuzi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuruhusu malori makubwa ya mizigo yaendelee kuzidisha uzito wa mizigo, umetajwa kuwa ni hatari na utaisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Hasara hiyo inatokana na uharibifu wa barabara za lami ambao unachangiwa kwa kiasi kikubwa na malori yanayozidisha uzito wa mizigo kinyume cha sheria na kanuni namba 7 (3) ya Sheria ya Usalama Barabarani ya 2001.
Ujenzi wa barabara ni wa gharama kubwa na hata ukarabati wake umekuwa ukitengewa mabilioni ya fedha za walipakodi kutokana na uharibifu unaofanywa.
Mathalani katika bajeti yake ya 2013/14, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, imetenga kiasi cha Sh314.535 bilioni kwa ajili ya mpango wa matengenezo ya barabara kuu na barabara za mikoa.
Kiasi hicho cha fedha ambacho ni zaidi ya robo ya bajeti nzima ya wizara hiyo kwa mwaka, kinatosheleza kujenga barabara mpya ya lami yenye urefu wa kilometa zipatazo 315, kwa makadirio ya kilometa moja kugharimu Sh1 bilioni. Katika mwaka huu wa fedha, bajeti nzima ya Wizara ya Ujenzi ni Sh1.226 trilioni.
Kauli ya Dk Magufuli
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, aliwahi kunukuliwa akisema ataendelea kusimamia sheria ya barabara namba 30 ya mwaka 1973, hadi anaingia kaburini kwa kuhakikisha hakuna magari ambayo yanazidisha uzito na kuharibu barabara.
“Nchini Ujerumani, uzito wa magari yote ni tani 40, Uingereza tani 40, Ufaransa 40, Urusi 38 lakini Tanzania tani 56, wakati mwingine tunakamata hadi tani 96,” alisema Dk Magufuli.
Hata hivyo, ujasiri wa Dk Magufuli ulizimwa na amri ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyetengua agizo la waziri huyo na kuamua kuruhusu magari yenye uzito uliopitiliza kuendelea kutumia barabara.
Wasemaji wa Serikali
Ofisa Habari wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo alisema suala hilo wameliachia Ofisi ya Waziri Mkuu. “Hilo suala liko Ofisi ya Waziri Mkuu, siwezi tena kulizungumzia,” alisema Ntemo kwa kifupi.
Hata hivyo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florence Turuka alisema siyo sahihi kusema kwamba Waziri Mkuu amevunja sheria kwani ilikuwa ni lazima serikali ichukue hatua jumuishi kwa kuwashirikisha wadau husika.
“Siyo sahihi kusema kuwa tunataka kuvunja sheria, sisi tumepokea mapendekezo na tutayaangalia kabla ya kutoa ripoti. Wewe vuta subira tu,” alisema Dk Turuka.
Dk Turuka alisema kamati iliyoundwa na Serikali ikiwajumuisha wadau mbalimbali wa barabara ilikamilisha kazi yake Desemba mwaka jana na kwamba hivi sasa Serikali inatafakari mapendekezo yaliyotolewa.
“Kamati ilishamaliza kazi tangu Desemba mwaka jana… tulipokea mapendekezo kwa sababu ile ilikuwa kamati jumuishi, kulikuwa na watu wa Tatoa, Taboa na Wizara ya Ujenzi na wataalamu, na sasa tunayafanyia kazi,” alisema Dk Turuka.
Baadhi ya barabara ambazo zilikuwa katika hali nzuri hivi sasa zimeharibika vibaya chanzo kikiwa ni uzito wa magari ya mizigo. Miongoni mwa hizo ni Barabara Kuu ya Morogoro - Dodoma kati ya Kijiji cha Magubike na Mji wa Gairo pamoja na Barabara ya Dar es Salaam ya Morogoro eneo la kati ya Mlandizi na Chalinze.
Hali hii ndiyo iliyomsukuma Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kufuta waraka unaoruhusu magari ya mizigo kuzidisha uzito na badala yake kutaka sheria inayotaka malori yanayozidisha uzito uliopo ndani ya asilimia tano kupunguza mzigo, kupanga mzigo upya au kulipia uzito uliozidi mara nne ya tozo ya kawaida, ifuatwe.
Uamuzi wa Dk Magufuli ulipingwa na wamiliki wa magari makubwa ya mizigo na kuungwa mkono na wamiliki wa mabasi ya abiria, hivyo Waziri Mkuu Pinda aliingilia kati na kuamuru utaratibu wa awali uendelee, ilhali suala hilo likiwa linatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.
Hata hivyo, Pinda alitangaza uamuzi wa kusitishwa kwa utekelezaji wa amri ya Dk Magufuli katika mkutano ambao hata hivyo waziri huyo wa sekta husika hakuhudhuria. Wakati huo kulikuwa na tishio la kusitishwa kwa usafirishaji nchi nzima kama amri hiyo isingetenguliwa.
Chanzo cha habari ndani ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kinasema: “Tatizo kuna viongozi wengi wenye malori na mabasi ndiyo wanaokwaza utekelezaji wa sheria hiyo.”
Kiliongeza: “Utakuta mtu ana magari hadi 300 na yote yanazidisha uzito kwenye barabara kwa kisingizio cha kusamehewa asilimia tano, unadhani barabara zetu zitaishia wapi? Ndiyo maana Dk Magufuli kwa uchungu aliamua kuweka msimamo”.
Takwimu za vipimo
Takwimu za upimaji wa magari ambazo ziko kwenye tovuti ya wakala huyo wa barabara nchini zinaonyesha kuwa licha ya kuwepo nafuu katika sheria bado magari mengi yamekuwa yakizidisha uzito.
Mathalan 2011/12 magari 684,600 yalipimwa na kati ya hayo, 167,310 sawa na asilimia 24.44 yalikutwa yakiwa yamezidisha mizigo, huku mengine 8,856 sawa na asilimia 1.30 yalipitisha kiwango cha asilimia tano.
Hata hivyo, inaelezwa katika taarifa hiyo kuwa, asilimia 98.67 ya magari yanayozidisha mizigo huwa katika kiwango cha uvumilivu wa asilimia tano, hali inayoonyesha kuwa ama wanahamisha mizigo au upangaji mbaya wa mzigo ule ule katika gari.
Kwa mwaka 2011/ 2012, Tanroads ilitoza fani ya Sh865,408,344.20 ambapo Sh859,508,181.40 zilikusanywa. Kwa mwaka 2013, magari 3,060,057 yalipimwa na kati ya hayo, 790,777 sawa na asilimia 25.84 yakiwa yamezidisha mizigo. Asilimia 1.62 yalikuwa ndani ya mstari wa asilimia tano na kwa jumla adhabu ya Sh5,490,255,235 ilikusanywa.
Wadau wa usafirishaji
Mkurugenzi wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Zacharia Hanspope alitetea mgomo wao huku akimtaka mwandishi amtafute msemaji wao kwa maelezo zaidi. Hata hivyo, alipotafutwa msemaji huyo, Elias Lukumay hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo akisema kuwa bado wako kwenye vikao na Serikali.
“Nisingependa kuzungumzia suala hilo kwa kuwa kwa sasa kuna vikao vinaendelea. Tutawajulisha tu,” alisema Lukumay.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo alisema kwa sasa wanaendelea na vikao na Serikali, lakini bado msimamo wao ni kutokubali kupima mabasi kwenye mizani.
“Tunaye mwakilishi wetu kwenye vikao na Serikali. Unajua kuna kamati iliyoundwa na Wizara ya Ujenzi na nyingine iliundwa na Waziri Mkuu,” alisema Mwalongo na kuongeza:
“Tumekuwa tukipinga hatua hiyo kwa muda mrefu. Mwaka 2004 tulipeleka madai serikalini na 2005 wakati Rais Jakaya Kikwete anaingia madarakani alitoa tamko la kutusitishia upimaji, lakini Wizara ya Ujenzi haitaki,” alisisitiza Mwalongo.
Sheria ilipindishwaje?
Ruhusa inayovunja sheria hiyo, ilitolewa na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Basil Mramba 2006, hatua ambayo iliwaudhi wafadhili kutoka Norway.
Katika barua yake aliyomwandikia Mwenyekiti wa Tatoa) wakati huo, S.A Seif, Julai 19, 2006 kujibu maombi yao, Waziri Mramba aliagiza kuwa gari lisionekane kuwa limezidisha uzito hata kama unazidi kiwango cha asilimia tano iliyowekwa na sheria hiyo.
“Kwa hiyo nimeamua kwamba, ekseli haitahesabika kuwa imezidisha kama mzigo huo utakuwa umepita kiwango cha kisheria baada ya kutoa asilimia tano cha uvumilivu wa kusoma mzani na baada ya kushuka hadi kilo 100,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Mramba ambayo gazeti hili limeiona..
Hata hivyo, barua hiyo ilipelekwa tu kama nakala Tanroads jambo linalodaiwa kumkera mkurugenzi wake. “Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads wakati huo, Ado Abeid alitaka sheria hiyo irudishwe kama ilivyokuwa, lakini Waziri Mramba alikataa,” kinasema chanzo cha habari.
Hatua hiyo ya kupindisha sheria inaelezwa kuwakera wafadhili wa barabara kutoka Norway, Kampuni ya Asborn Norwegian Public Roads Administration iliyokuwa ikishauri kuhusu udhibiti wa uzito na hivyo kujitoa tangu mwaka 2006 kwa kutoridhishwa na hatua hiyo.
Sehemu ya barua hiyo ya Novemba 18, 2006, inasomeka: “Baadhi ya vipengele vilivyomo katika barua vinahusika na vinatakiwa kufuatwa kama hatua muhimu za kuimarisha utendaji wa mizani, kanuni na vitendea kazi.
“Hata hivyo, barua yako pia imezungumzia mambo ya kufanya kuhusu udhibiti wa mzigo katika ekseli ambapo baadhi ya vipengele vimeachwa. Hali hii itaathiri udhibiti kwa ujumla na kusababisha vurugu na uharibifu utakaoathiri utendaji.”
Kwa mujibu wa chanzo hicho, baada ya barua hiyo na kutokuwepo kwa dalili ya kurekebisha sheria hiyo, tangu wakati huo kampuni hiyo ilijitoa kusaidia miradi ya barabara nchini.
Hata hivyo, uamuzi wa Mramba uliopata utetezi wa Pinda alipokuwa akitengua amri ya Dk Magufuli akisema ilitokana na malalamiko ya wadau.
“Lengo lake ilikuwa ni kufidia matatizo ya upungufu wa mizani kutoweza kupima kwa usahihi uzito wa magari yanayopimwa katika vituo mbalimbali vya mizani nchini, lakini hivi sasa mizani yetu ni mizuri na ya kisasa,” alisema Pinda na kuongeza:
“Lakini ikumbukwe kuwa agizo hilo lilikuwa kinyume na Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 toleo la 2002 na kanuni zake za 2001, ambayo inazuia malori kuzidisha uzito. Mramba aliamua vile ili kumaliza hali iliyokuwa imejitokeza wakati akiwa Wizara ya Miundombinu”.
Chanzo kinaendelea kufafanua kuwa, baada ya Mramba kuondoka katika wizara hiyo mwaka 2007, wizara hiyo pia iliongozwa na mawaziri, Andrew Chenge na Dk Shukuru Kawambwa ambao pia hawakuwahi kuifanyika kazi sheria hiyo.
Matakwa ya sheria
Sheria Na. 30 ya 1973 na kanuni Namba 30 ya 2001 iliyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali tangazo Namba 30 la Februari 9, 2001 ilianza kutumika Januari 24, 2001 inafafanua uzito wa magari unaotakiwa.
Kipengele cha saba cha sheria hiyo kinaeleza magari yote yenye uzito kuanzia tani 3.5 na kuendelea na aina ya makosa ya uzidishaji uzito, ambapo kifungu cha 2, 3, 4 vinafafanua matumizi ya uzito uliozidi asilimia tano.
Vifungu vya sheria hiyo vinasomeka ifuatavyo:
2. Kwa sababu ya usambazaji wa mzigo kwenye gari, ekseli au fungu la ekseli litahesabika kuwa limezidi uzito kama mzigo utazidi ukomo wa uzito unaoruhusiwa kisheria baada ya kuongeza asilimia tano (5) ya uzito unaoruhusiwa, na kisha kuiweka hesabu ya mwisho isomeke kwa wastani wa kilo mia moja za karibu.
3. Kwa kila ekseli yaweza kusafirisha kama ziada ya uzito kiasi cha asilimia tano (5) ya uzito unaoruhusiwa. Hata hivyo, kama mzigo wenye uzito wa ziada hautapakuliwa, tozo kwa uzito huo wa ziada itakuwa mara nne zaidi ya tozo ya kawaida inayolipwa kwa uzito uliozidi.
Mzigo wote wenye uzito unaozidi asilimia tano (5) utapakuliwa na kupakiwa kwenye gari jingine isipokuwa tu kama kibali maalum kimetolewa.”
4. Kama gari limethibitishwa kwamba limebeba uzito zaidi ya ule unaoruhusiwa gari hilo halitaruhusiwa kuendelea na safari mpaka hapo mzigo uliozidi utakapohamishiwa kwenye gari lingine au kupangwa upya ili kila ekseli iwe na uzito unaotakiwa.
“Baada ya kushusha au kupagwa upya gari lazima lipimwe upya tena kuhakikisha kuwa mzigo uliobebwa upo kwenye viwango vinavyokubalika.”