Serikali ya Sudan Kusini inasema imeukomboa mji wa Bor, mji muhimu ambao umedhibitiwa mara na serikali na mara nyingine na wapinzani wa serikali tangu mgogoro kuzuka katikati ya Desemba.
Msemaji wa serikali Philip Aguer anasema majeshi ya SPLA yaliingia Bor Jumamosi na kuwashinda wapiganaji wa upinzani wapatao 15,000. Alisema jeshi limezuia mpango wa makamu rais wa zamani Riek Machar wa kushambulia mji mkuu wa Juba.
Hapakutolewa tamko la mara moja na upande wa wapiganaji wa upinzani juu ya hali ya mji wa Bor, mji mkuu wa jimbo la Jong’lei.
Shirika la ukanda huo la mamlaka za serikali na maendeleo IGAD linajaribu kupatanisha pande zote mbili kusitisha mapigano, katika mkutano nchini Ethiopia baina ya wawakilishi wa serikali na wanaoipinga serikali.