Wakimbizi waliyohama makaazi yao, nchini Jamhuri ya Afrika ya KatiRFI
Na RFI
Umoja wa Mataifa unaonya kuwa huenda kukatokea na mauji ya kimbari katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiwa suluhu la haraka la kisiasa halitapatikana. Wabunge kesho Jumamosi wanatarajiwa kumchagua rais wa mpito baada ya kujiuzulu kwa Mitchel Djotodia na waziri wake mkuu Nicolas Tiangaye, licha ya kuondoka Kwa viongozi hao wawili, vita vinaendelea kuripotiwa mjini Bangui na watu saba waliuawa jana.
John Ging mkurugenzi mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na misaada ya kibinadamu OCHA amekuwa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na amesema kama Jumuiya ya Kimataifa haitaingilia kati na kutafutia ufumbuzi mgogoro unaoripotiwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, nchi hio inaweza kujikuta imeingia katika dimwi la machafuko.
Nalo Shirika la Kimataifa la kushughulikia mizozo la International Crsis Group linaonya kuwa huenda machafuko ya kidini kati ya Waislamu na Wakiristo yakaendelea kushuhudiwa.
Tibot Lesfer mtafiti wa shirika hilo, amesema Kuna hatari ya machafuko makubwa ambayo yana msingi wa kidini na hatari ya hivi karibuni ni kwamba waislamu wanaweza kulengwa kwa sababu wanahusishwa na vuguvugu la seleka.
Wakti huhuo, zoezi la kuuandaa uchaguzi wa rais mpya unaendelea, huku kesho ikiwa ndio siku iliyopangwa kufanyika kwa uchaguzi huo. Jumuiya ya kimataifa imeendelea kuwashinikiza viongozi wa mpito kuharakisha zoeazi hilo la uchaguzi ambalo hata hivyo huenda likasogezwa mbele kati ya Jumapili na Jumatatu.
Hali ya utulivu imeanza kurejea hatua kwa hatua licha ya kuripotiwa vitendo kadhaa hapa na pale vya mauji katika baadhi ya mitaa ya jiji la Bangui.
Awali luteni Konaté mmoja wa viongozi wa wanamgambo wa anti-balaka, alisema mchakato wa kumtafuta rais mpya unaoendelea bungeni na unaonekana kuegemea upande mmoja kiasi cha kutowaridhisha.
“Sisi anti-balaka ambao tumesababisha mabadiliko hayo hatutachoka kusema kuwa taasisi hizo zilizoundwa na baraza la taifa zinajaa na watu ambao wameteuliwa na Djotodia na Tiangaye. Tunaomba kuwepo na muundo mpya na Bunge hilo, lazima mabadiliko yawe katika bunge”, amesema Luteni Konaté.
kwa upande wa waasi wa zamani wa Séléka, wao walisema hali ni tulivu na wapo tayari kuweka silaha chini na kushirikiana na rais mpya ataye chaguliwa.
Jenerali Ba kiongozi wa waasi wa zamani wa sélékas, alifahamisha kwamba watashirikiana na rais mpya wa mpito.
“Ikiwa Djotodia ameondoka sio mwisho wa dunia, waseleka hawapo hapa kwa ajili ya Michel, ni wananchi ambao wako tayari kushirikiana na serikali mpya pamoja na rais mpya wa mpito, na tunaweza kufanya kazi na wapinzani wetu, tunajuana, lazima tufanye kazi pamoja”, amesema jenerali Ba.
Wakati huohuo, wafadhili wa kimataifa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaendelea kushinikiza Baraza la Kitaifa la Mpito la nchi hio (CNT), ambalo ni bunge la mpito, kutoidhinisha majina ya watu kutoka upande wao watakaogombea kwenye uchaguzi ujao wa rais wa muda unotazamiwa kufanyika jumamosi.
“Jumuiya ya Kimataifa imelitaka Baraza la Kitaifa la Mpito kutochukua uamzi wowote unaohusiana na mchakato wa kumchaguwa rais mpya wa mpito”, amesema jenerali Noël Essongo, muakilishi wa msuluhishi katika mzozo wa Jamuhuri ya afrika ya Kati, rais wa Congo Denis Sassou Nguesso, akiwa pia mwenyekiti wa kamati ya ufundi inayofuatilia mchakato wa wa amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kamati hiyo inaundwa na Jumuiya ya Kimataifa, ikimaanisha wafadhili wa Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mzozo unaoikumba nchi hio, ikiwemo Ufaransa, Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Uchumi ya Mataifa ya Afrtika ya Kati (CEEAC).
Hivi karibuni Jumuiya ya kimataifa ilitolea wito Baraza la Kitaifa la Mpito ichangie kwa kutoa masharti yanayohitajika na kutoruhusu watu wake kugombea kwenye uchaguzi, ambao utakua huru na wa haki, amesema jenerali Essongo katika tangazo liliyotolewa na ofisi ya msuluhishi.
Tangazo hilo linabaini kwamba ofisi ya msuluhishi na Jumuiya ya Kimataifa vimepongeza juhudi za Baraza la Kitaifa la Mpito, ambalo limekua likiandaa uchaguzi ili kumpata haraka iwezekanavyo rais wa mpito.
Hata hivyo, rais wa mpito, Alexandre-Ferdinand Nguendet, aliechukuwa nafasi ya Michel Djotodia aliejiuzulu hivi karibuni, alibaini hivi karibuni kwamba hatagombea kwenye uchaguzi ujao ili kuepusha hali ya wasiwasi ambayo inaweza kujitokeza kutokana na kugombea kwake, na ataendelea kushirikiana na wengine kwa ujenzi wa taifa.
Mikataba ya kimataifa inapendekeza kua rais wa mpito hapashwi kugombea kwenye chaguzi za mwaka 2015.