Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mbeya jana, Mangula alisema kuwa wote wanaovunja kanuni za uchaguzi kwa kutangaza nia kabla ya wakati, hawataweza kuteuliwa kuwania uongozi katika uchaguzi mkuu mwakani.
Ingawa Mangula hakutaja jina la Lowassa, lakini kauli yake dhahiri ilikuwa ikimlenga mbunge huyo ambaye amekuwa akishambuliwa na makada maarufu wa CCM kwamba amevunja kanuni.
Katika mkutano huo, Mangula alisema CCM imeshtushwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya makada wake kwa kutofuata kanuni na maadili ya chama hicho.
Alisema inasikitisha kuona kuwa licha ya kukomaa kwa demokrasia, makada hao wanatumia fursa hiyo kutoa maoni yao kwa kuvunja maadili.
Kauli hiyo inakuja katika kipindi ambacho baadhi ya makada wakiwamo vigogo wastaafu wa chama hicho wamekuwa wakitoa kauli za kukemeana kutokana na baadhi yao kudaiwa kuvuruga chama hicho kwa sababu ya harakati za uchaguzi wa 2015.
Akizungumza kuhusu yanayoendelea CCM, Mangula alisema anashtushwa na namna ambavyo makada na wanachama wanashindwa kuzingatia kanuni za chama.
“Kinachoendelea ndani ya chama hicho ni mshtuko na mshangao wa uvunjwaji wa kanuni na utaratibu unaofanywa na baadhi ya makada wetu,” alisema Mangula ambaye yupo mkoani hapa kwa ajili ya CCM.
Alisisitiza ni muhimu kwa wanachama wa ngazi zote kuzingatia kanuni na maadili yaliyowekwa na chama hicho katika kufanya mambo yake.
“Ni wajibu kwa kila mwanachama kutambua kanuni na taratibu ziliwekwa na chama. Inashangaza kuona kanuni zipo, lakini wanaotoa maoni yao wanashindwa kuzifuata.
“Kinachoshangaza ni msigano unaoendelea katika hao ambao wamepata uhuru wa demokrasia katika kutoa maoni yao kuhusu chama,” alisema Mangula.
Hata hivyo, Mangula alisema jambo la kufurahisha ni kuona chama kimekuwa na afya ya demokrasia ambayo inatoa nafasi ya kujadili na kuchambua mambo kwa kina na kwa uhuru.
Kuhusu uhai wa chama kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2015, alisema kimejipanga vizuri na kwamba kitashinda kwa kishindo.
Alisema hawana tatizo na chama ambacho kina wanachama zaidi ya milioni sita na wafuasi walio imara katika kuhakikisha kinashinda.
Mangula ambaye pia ni mlezi wa Mkoa wa Mbeya, alitumia nafasi hiyo kusisitiza kuwa CCM imekuwa na utaratibu mzuri wa kufanya shughuli zake, na hiyo ndiyo iliyofanya mwaka huu maadhimisho ya miaka 37 kufanyika mkoani hapa.
Akizungumzia siasa katika Mkoa wa Mbeya, Mangula alisema wamepoteza majimbo mawili, lakini hata kama wangekuwa hawajapoteza, bado ni wajibu wao kutafakari namna ya kuimarisha chama na kuendelea kushika dola ili kuwatumikia Watanzania kuwaletea maendeleo.
UVCCM wamgeuzia ‘kichapo’ Malecela
Katika hatua nyingine, Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), mkoani Morogoro wameelezwa kushangazwa na kauli ya Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu Mwenyekiti, John Malecela kwa uamuzi wa kumuunga mkono Paul Makonda kumshambulia Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM).
Mbali na hilo, wamemtaka Malecela kuacha kumtuhumu Lowassa kwa kuchangia harambee, kugawa tisheti na kutoa misaada katika nyumba za ibada na kuwaacha wanachama wengine wanaofanya hayo wakiwemo Bernard Membe, Fredrick Sumaye, Samuel Sitta na January Makamba.
Taarifa iliyosambazwa jana katika mitandao ya kijamii na kada wa umoja huo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza la Umoja wa Vijana mkoani humo, Heri Hoza, ilisema kuwa CCM inapaswa kupiga marufuku matamko yanayoendelea kutolewa kiholela na wanachama wake.
Alisema wanamuomba Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Jakaya Kikwete kukemea hali hiyo ili kukinusuru chama ambacho hivi sasa kinaonekana kuyumbishwa na makundi ya urais.
Kada huyo alisema ni vyema viongozi wa chama hicho kuacha kukaa kimya kwani ukimya huo unazidi kukuza mpasuko na makundi ndani ya chama hicho tawala.
Hoza alisema Makonda amekiuka Katiba ya CCM Ibara ya 14(4) inayosema mwanachama yeyote atakuwa na haki zifuatazo: “Haki ya kujitetea au kutoa maelezo mbele ya kikao cha CCM kinachohusika katika mashtaka yoyote yaliyotolewa juu yake, pamoja na haki ya kukata rufaa kwenda katika kikao cha juu zaidi cha CCM kama kipo endapo hakuridhika na hukumu iliyotolewa.”
Alihoji kuwa ni lini CCM iliwahi kumuita Lowassa na wengine wenye kashfa za rushwa na walioonyesha nia ya urais kwa ajili ya kuwahoji na kuwasikiliza na chama hicho kikatoa uamuzi?
Alisema tamko la Makonda lililotolewa kwa kofia ya chama dhidi ya Lowassa limeonyesha kuwa kada huyo anapaswa kwajibishwa.
“Tunamshangaa Malecela kuunga mkono mtu aliyekiuka haki za mwanachama na utaratibu wa chama. Huu ni ukweli kuwa tegemeo la wazee wa CCM kusimamia haki na wajibu wa chama umetoweka,” alisema.
Hoza alisema Makonda aliwakashifu viongozi wa dini kwa kuwafananisha na wasaka pesa, hivyo wanamtaka awaombe radhi viongozi hao.
“Je, Malecela anaunga mkono Makonda kuwakashifu viongozi wa dini? Tulitegemea mzee huyo angekemea matendo haya kwa wanachama wote, lakini ameonyesha chuki binafsi kwa Lowassa.
“…Hatupaswi kumshangaa maana hata Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliposema kama Malecela atagombea urais anarudisha kadi ya CCM, hatukumuelewa alikuwa akimaanisha nini, lakini sasa tumepata picha kamili jinsi mzee huyu alivyokosa busara na anaweza kukizamisha chama kwa chuki zake binafsi na maneno yake ya kupotosha Watanzania,” alisema.
Alisema Malecela anapaswa pia kuomba radhi UVCCM kwa kumuunga mkono Makonda ambaye si msemaji wa jumuiya hiyo kwa mujibu wa kanuni.
Kuhusu wanachama wengine wa CCM kuanza kampeni, mwenyekiti huyo alisema kuwa baadhi ya wanachama wametengeneza kalenda kama sehemu ya kujinadi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hoza alisema anashangazwa kwa nini chama kimeacha kuwakemea wanachama hao wote kwa umoja na badala yake anaandamwa Lowassa pekee.