Nape amchokonoa Rostam

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema moja ya magamba yaliyovuka katika chama hicho ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.
Nape aliyasema hayo jana alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari mkoani Mbeya, baada ya kueleza ujio wa Rais Jakaya Kikwete mkoani hapa kwa ajili ya kuadhimisha miaka 37 ya kuzaliwa CCM.

Alisema anakiri kuwa chama hicho hakipo sawa kwa asilimia 100, huku akikifananisha na nyumba yenye ufa, hivyo uwezekano wa kukarabati ni mkubwa kuliko ungepasuka msingi.

Alipoulizwa kuwa uongozi wa CCM unafuta historia ya chama chao kwa kusherehekea kuzaliwa kwake tarehe ambayo hakikuzaliwa, alisema siyo mara ya kwanza kufanya hivyo.

“Tutaadhimisha Februari 2 mwaka huu ili kuwapa nafasi hata wafanyakazi kuhudhuria maandamano ya mshikamano yatakayoongozwa na Rais Kikwete wala siyo kufuta historia,’’ alisema Nape.

Alisema tayari viongozi wa chama hicho wameanza kuwasili mkoani hapa ambapo kesho watafanya maandamano kutoka Soweto hadi ofisi za CCM mkoa, kisha wataelekea Uwanja wa Sokoine.

“Sherehe zetu zitaambatana na shughuli za kijamii, ikiwemo kujenga zahanati, kupanda miti maeneo ya vyanzo vya maji na zitaonyeshwa na vituo vitatu vya luninga na kutangazwa na redio,” alisema katibu huyo aliyepata kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mtwara.

Alipotakiwa kujibu maswali kuhusu minyukano ya malumbano kwenye vyombo vya habari kwa wanachama na viongozi wao, alisema kila mtu anao uhuru wa kuzungumza lolote.

Nape aliwaomba waandishi wa habari kuyaweka maswali yao huku akiahidi kuyajibu Februari 3, likiwemo suala la mambo waliyomshauri Rais Kikwete kuhusu mawaziri mizigo ambao katika uteuzi wa hivi karibuni uliofanywa na rais, waliendelea kuwepo madarakani.

“Hivi kati yenu nani anayejua tulichomshauri rais kuhusu mawaziri hao? Kama yupo anyoshe kidole maana suala la ushauri ni siri, hivyo naombeni maswali mengine niyajibu tarehe 3,’’ alisema Nape.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company