Bunge: Watanzania wasubiri miujiza leo, Wajumbe wafika njia panda upigaji wa kura , CCM wang`angana na ya wazi, wengine ya siri

NA WAANDISHI WETU

Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba,Pandu Ameir Kificho.
Misimamo isiyoyumba juu ya namna ya upigaji kura ndani ya Bunge Maalum la Katiba ama ya siri au wazi ambayo imewagawa wajumbe katika msingi ya kiitikadi, leo inatarajiwa kuamualiwa katika hali inayotishia mustakabali wa kupatikana katiba mpya nchini.

Bunge leo linatarajiwa kupokea taarifa kutoka kwa Kamati ya Maridhiano kuhusu utaratibu wa kupiga kura za wazi au siri utakaotumiwa kupata uamuzi wa kupitisha Rasimu ya Katiba, huku tayari misimamo hiyo miwili ikiwa imejitenga kama mbingu na nchi.Kupatika kwa mwafaka sasa ni miujiza kutokana na mgawanyiko huo ambao unaakisi itikadi za vyama, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikidaiwa kujiapiza kwa msimamo wa kura ya wazi, huku wajumbe wengine hawa wa vyama vya upinzani wakitaka kura ya siri.

Uchunguzi wa NIPASHE ndani ya safu ya wajumbe wa Kamati ya Maridhiano iliyoundwa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba, Pandu Ameir Kificho, umethibitisha kuwa hadi kufikia jana jioni hakuna kikao chochote kilichokaa kujadili mgawanyiko juu ya kifungu cha 37 na 38 vya rasimu ya kanuni za bunge hili zinazobishaniwa zikizungumzia mfumo wa upigaji kura na akidi ya upigaji kura.

“Kamati haijakutana tangu Mwenyekiti wa Muda (Pandu Ameir Kificho), alipoahirisha semina ya wajumbe ya kujadili Kanuni za Rasimu ya Katiba juzi usiku na kuahidi kuwa itakwenda kusaka mwafaka na kuwasilisha taarifa wakati Bunge litakapokutana kesho (leo) saa 5:00 asubuhi,” alisema mjumbe mmoja wa kamati hiyo.

Wajumbe wengi hasa kutoka CCM wanapinga kanuni ya 37 na 38 ya Rasimu ya Kanuni inayopendekeza utaratibu wa kufikia maamuzi uwe wa kura ya siri, na badala yake wanataka utaratibu wa kura ya wazi utumike.

Iwapo wajumbe wa Bunge Maalum watafikia mwafaka wa taarifa itakayotolewa na timu hiyo na kuridhia, basi Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum zinaweza kupitishwa leo, lakini kama hakutakuwa na mariadhiano hayo, Bunge Maalum litakuwa njia panda kuhusu namna ya kupata uamuzi wa kupitisha Rasimu ya mwisho ya Katiba.

Wajumbe wa Kamati ya Maridhiano yenye wajumbe mashuhuri na wenye busara ili kutafuta mwafaka kwa kanuni ambazo wajumbe wanatofautiana ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Kificho mwenyewe.

Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi; Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar; Mohammed Aboud; Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Bunge, Profesa Ricky Mahalu; Naibu Katibu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai na Kingunge-Ngombale Mwiru.

Pia wamo Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba; Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia; Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo; Dk. Tulia Ackson; Olive Luena; Sheikh Thabit Nouman Jongo; mkuu wa Kanisa la Anglikana mstaafu, Donald Mtetemelwa; Peter Kuga Mziray; Salma Haji Saadat na Fatma Himid.

Vyanzo vyetu kutoka ndani ya kamati hiyo vimeeleza kuwa kati ya juzi na jana hakuna kikao chochote kilichofanyika kusaka mwafaka, hivyo kuna uwezekano mkubwa semina ya Bunge ya kujadili kanuni isifanyike leo asubuhi.

Mmoja wa watoa taarifa, alisema kuwa jana Kamati Kuu (CC) ya CCM ilikuwa inakutana, hivyo isingekuwa rahisi kwa Kamati ya Maridhiano kufanyika kutokana na wajumbe wake wengi kuwa wajumbe wa CC. Miongoni mwao ni Pinda, Kificho, Lukuvi na Vuai.

“Tunatarajia kukutana kesho (leo) asubuhi kwa kuwa semina ya Bunge la Katiba kuhusu kanuni itaanza saa tano,” alisema mjumbe huyo.

“Kanuni mbili ndiyo zimezua mjadala mkubwa na tumekubaliana ziachwe kwanza na semina iendelee kujadili na kupisha kanuni nyingine, kesho (leo) Kamati ya Maridhiano itakutana tena katika harakati zake za kutafuta mwafaka,” alisema wajumbe mwingine wa kamati hiyo.

Taarifa ambazo zililifikia NIPASHE jana jioni zilieleza kuwa CCM bado wanashikilia msimamo wa kutaka utaratibu upigaji kura uwe wa wazi huku wabunge wa upinzani wakipinga utaratibu huo na wajumbe 201 wanaotokana na asasi na makundi mbalimbali wakiwa wamegawanyika katika suala hilo.

Ugumu wa kamati hiyo kupata mwafaka pia unatokana na msimamo wa upinzani kwamba wataendelea kupigania kura ya siri.

Mmoja wa wajumbe kutoka vyama vya upinzani aliliambia NIPASHE kuwa: “Utaratibu wa kupiga kura ya siri ni haki ya msingi na siyo msimamo wa kundi fulani. Sisi tutaendelea na msimamo wa kupigania kura ya siri.”

Kutokana na msimamo hyo kinzani, ni dhahiri kuwa ratiba za Bunge hilo inazidi kuchelewa likiwa linaingia wiki ya nne hata kabla ya kukubaliana juu ya utaratibu wa upigaji kura katika kupitisha katiba mpya.

Kuna habari kwamba wabunge wa CCM mwishoni mwa wiki walikutana mara kadhaa kuweka msimamo usiyoyumba kwamba wanataka kanuni za Bunge Maalum la Katiba ziseme wazi kuwa kura zitapigwa kwa uwazi na siyo za siri.
CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company