Mjumbe wa Bunge maalumu la Katiba, Chritopher Ole Sendeka
Na Daniel Mjema na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, juzi na jana wamekuwa katika mtihani mgumu wa kufikia uamuzi wa pamoja kuhusu utaratibu wa upigaji kura, kati ya kura ya wazi na kura ya siri.
Habari kutoka katika kikao cha ndani cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), zilisema kutokana na mvutano huo, mjumbe mmoja, Chritopher Ole Sendeka, alijikuta akilia hadharani akitetea upigaji kura ya wazi.
Kikao hicho kilichofanyika juzi kati ya saa 2:00 na saa 5:30 usiku chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kilishuhudia mabishano makali kati ya wanaotaka kura ya siri dhidi ya wale wanaotaka kura ya wazi.
Habari hizo zilisema baada ya Pinda kufungua kikao hicho, alimkaribisha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Shamsi Vuai Nahodha, ili atoe mrejesho wa kikao cha mashauriano.
Inaelezwa kuwa katika kikao hicho, Nahodha aliwaambia wajumbe kuwa kutokana na mazingira yaliyopo ndani na nje ya Bunge kwa upande mmoja na wananchi kwa upande mwingine, kura ya siri haiepukiki.
“Kilio cha Ole Sendeka kwenye party cocas kikao cha chama (party cocus) juzi usiku kilitokana na kauli ya Nahodha kwamba kura ya siri haiepukiki,” alidokeza mbunge mmoja wa CCM aliyehudhuria kikao hicho cha faragha.
Mbunge huyo alilidokeza gazeti hili kuwa ndani ya kikao kulikuwa na mabishano makali baada ya kauli ya Nahodha, huku baadhi ya wabunge wakisema wananchi wamechoshwa na msimamo wa CCM.
Ni kutokana na mabishano hayo ndipo Ole Sendeka aliposimama akipinga mapendekezo yaliyotaka CCM kulegeza msimamo na kuridhia kura ya siri na wakati alipokuwa akizungumza alipobubujikwa na machozi.
Huku akilia katika kikao hicho, inadaiwa Ole Sendeka akisema kwamba kukubali kura ya siri ni kuitosa CCM na msimamo wake wa kutaka muundo wa Serikali mbili.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilidai kuwa Ole Sendeka alienda mbali zaidi na kusema endapo Pinda ataridhia kura hiyo ya siri, basi yeye (Pinda) na viongozi waandamizi wa CCM waliohudhuria watawajibishwa na CCM.
Kutokana na mtafaruku huo, kikao hicho kilishindwa kufikia mwafaka na kuahirishwa hadi jana saa 5:00 asubuhi ambapo hoja ya ama kura ya siri au ya wazi, iliendelea kuwagawa wabunge katika makundi mawili.
Wakati akifungua kikao cha jana, Pinda alisema kutokana na yaliyotokea katika kikao chao cha juzi usiku na baada ya kutafakari kwa mapana yake, chama kimeamua kibakie na msimamo wake wa kura ya wazi.
“Kutokana na yaliyojitokeza jana (juzi) na hasa ukiona mtu mzima analia, tumetafakari tumeona tubaki na msimamo wa kura ya wazi,” alisema mmoja wa wabunge akimkariri Waziri Mkuu Pinda.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, katika kikao hicho ilielezwa kuwa kukubali upigaji kura wa siri ni kuiua CCM kwa sababu wajumbe wengi wa Bunge Maalumu la Katiba, watapitisha muundo wa Serikali tatu badala ya mbili.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wamehoji kitendo cha Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho kuhudhuria kikao cha ndani cha wabunge wa CCM.
“Kificho ni mwenyekiti wa Bunge lenye makundi tofauti, sasa anapoingia kwenye kikao cha wabunge wa CCM kinachoweka mikakati ya kupingana na makundi mengine anatoa picha gani?” alihoji mbunge mmoja.
Taarifa za Kificho kuhudhuria kikao hicho cha jana cha CCM zilionekana kuwakera wajumbe wengine wa Bunge hilo, wanaotokana na vyama vya upinzani na wale wanaotoka katika kundi la wajumbe 201.
“Bado tunatafakari tuchukue uamuzi gani, lakini tukiona vipi, tutasusia kikao cha leo (jana) jioni, nyie njooni ndani lolote linaweza kutokea,” alidokeza mjumbe huyo anayetoka katika kundi la vyama vya hiari.
Kura ya siri, wazi yawekwa kiporo
Hata hivyo, jana mara baada ya Kificho kuanza kikao cha semina saa 10:40 alasiri badala ya saa 9:00 alasiri alisema semina hiyo imechelewa kuanza kwa sababu ya masuala muhimu.
Kificho aliwaambia wajumbe kuwa kamati ya mashauriano ilikuwa imemshauri kanuni ya 37 na 38 zinazohusu kura ya siri viwekwe kiporo kutokana na kutopatikana kwa mwafaka.
“Kamati imenishauri bado tuache kanuni ya 37 na 38 ili kamati ya mashauriano iendelee kunishauri vizuri zaidi ili baadaye tuje tuwaambie kamati ya kanuni iziandike vipi,” alisema.
Kutokana na ombi hilo, wajumbe waliafiki waendelee kupitia kanuni ya 32 hadi 36 na 39 hadi 43 ambavyo havina mvutano.
UKAWA waweka msimamo
Katika hatua nyingine, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA), wameweka msimamo wa pamoja wa kutaka kura ya siri.
Umoja huo unaojumuisha vyama vyote vya upinzani ndani ya Bunge hilo, walikutana jana kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi saa 8:30 mchana katika ukumbi wa Pius Msekwa.
Mkutano huo uliwajumuisha pia Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba.
Mbowe alipoulizwa jana alisema msimamo wa umoja huo bado umebakia kura ya siri, akisema utaratibu huo ndiyo mwafaka utakaowawezesha wajumbe kupiga kura bila kuingiliwa.
Walioteuliwa na Rais wakwama
Kwa upande wa kundi la wajumbe 201 walioteuliwa na Rais, juzi walikubaliana kila kundi liteue watu watatu wataokwenda kukutana na kamati ya mashauriano ndipo waweke msimamo.
Taarifa zilizopatikana baadaye jana zilieleza kuwa kundi hilo lilimchagua Dk Francis Michael kuwa mwenyekiti, halafu makundi madogo madogo yatateua viongozi kuunda kamati ya utendaji.
Kamati hiyo ya viongozi ndiyo itakayokutana na Kamati ya Mashauriano ili kuweza kukubaliana kuhusu kanuni za 37 na 38 zisomekeje.
Imeelezwa kuwa hadi semina ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba inaanza saa 10:40 alasiri walikuwa hawajakutana na kamati ya mashauriano.