Kuala Lumpur. Polisi nchini Malaysia wamevamia nyumba aliyokuwa akiishi rubani wa ndege iliyopotea na kuendesha msako mkali, ikiwamo kukusanya nyaraka muhimu ambazo zinazamiwa kuwa zitasaidia kufichua ukweli kuhusu tukio la kupotea kwa ndege hiyo.
Ripoti zilisema kuwa upekuzi huo, ambao pia umefanyika katika nyumba aliyokuwa akiishi rubani msaidizi, umefanyika baada ya kuibuka kwa taarifa zinazodai kuwa rubani huyo, Zaharie Ahmad Shah alikuwa na mrengo wa siasa kali.
Shah alikuwa ni shabiki na mfuasi wa wazi wa mwanasiasa wa upinzani, Anwar Ibrahim ambaye sasa yupo gerezani baada ya kukutwa na hatia ya kujihusisha na vitendo vya fedheha.
Inaaminika kuwa rubani huyo alikuwapo mahakamani wakati mwanasiasa huyo alipopandishwa kizimbani mwezi Machi mwaka huu na pengine hakufurahishwa na hukumu hiyo.
Kwa sasa polisi wanashikilia nyaraka kadhaa, ikiwamo kompyuta ambayo inadhaniwa kuwa na taarifa muhimu zilizohifadhiwa na rubani huyo.
Polisi hao wameenda mbali zaidi kwa kuanzisha uchunguzi wa kimazingira ambao utasaidia kupata historia binafsi kuhusu maisha ya rubani huyo aliyetajwa kuwa na uzoefu mkubwa wa urushaji wa ndege.
Wataalamu wa saikolojia na wale wanaohusika na usalama wa anga wameitwa kuongeza nguvu ili kusaidia kuchambua taarifa zinazoendelea kukusanywa kuhusu mwenendo wa rubani Shah ambaye nyumba yake bado inaendelea kulindwa.
Kitendo cha polisi kuifanyia upekuzi nyumba ya rubani huyo pamoja na kukusanya taarifa zake binafsi kimeelezwa kwamba ni jitihada za Serikali kutaka kujiridhisha hasa kutokana na mazingira yanayohusisha upotevu wa ndege hiyo.
Wachunguzi hao wanataka kujua kama kumekuwa na tukio lolote la matatizo ya kiakili na kumewahi kujitokeza kwa changamoto za kifamilia kwa marubani hao au kwa yeyote aliyekuwamo kwenye ndege hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Kuala Lumpur na kuelekea Beijing.
Pamoja na kwamba marubani wa ndege hiyo ya Malaysia walikuwa na rekodi nzuri, kuna wasiwasi pengine walikutwa na tukio lililosababisha kujiingiza kwenye hali ambayo ingepoteza umakini wa kuongoza ndege.
Uchunguzi pia unawalenga abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo iliyokuwa na umri wa miaka 11 na kwamba hatua hiyo inaweza kusaidia upatikanaji ukweli halisi juu ya tukio hilo.
Serikali yaomba msaada
Malaysia imeomba msaada zaidi kutoka nchi kadhaa kwa ajili ya kusaidia kuitafuta ndege hiyo ya abiria iliyopotea kwa zaidi ya wiki moja iliyopita huku kukiwa na taarifa za kusitishwa uchunguzi kwenye Bahari ya Hindi mpaka pale tathimini ya kina itakapofanyika.
Wizara ya uchukuzi ilisema kwamba imeomba msaada kutoka nchi za Kazakhstan, Uzbekistan, Kyrgyzistan, Turkmenistan na Pakistan. Nchi nyingine zilizoombwa kushiriki ni pamoja na Indonesia, Thailand, Marekani, Australia na Ufaransa.
Msaada huo ni pamoja na takwimu za Satelaiti zilizonasa safari ya ndege hiyo iliyokuwa na watu 239 na ambayo ilipotea tarehe 8 mwezi huu, baada ya kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kuala Lumpur.
Awali Waziri Mkuu wa Malaysia, Najib Razak alisema wachunguzi waligundua kwamba ndege hiyo, iliyokuwa ikielekea Bejing nchini China, ilibadili njia na kuelekea Magharibi kabla ya mitambo yake ya mawasiliano kuzimwa.
Akizungumza na waandishi habari katika mji mkuu wa Kuala Lumpur, Najib Razak alisema: “Wachunguzi wanaamini kwa kiwango kikubwa kwamba kulikuwa na kitendo cha makusudi cha kuzima mfumo wa mawasiliano katika ndege aina ya Boeing 777-200ER ya shirika la ndege la Malaysia Airlines.
Kwa msingi huo, ndege hiyo haingeweza kuwasiliana na kituo cha kudibiti trafiki angani.”
Waziri Mkuu wa Malaysia aliongeza kuwa baada ya kuzimwa mfumo huo wa mawasiliano, ndege hiyo ilibadilisha mkondo wake na kuelekea upande wa Magharibi baharini jambo ambalo linaashiria kulikuwa na hatua za makusudi.
Alisema pamoja na kuwepo taarifa kuwa ndege hiyo ilitekwa nyara, bado hakuna lolote lililo wazi kwani uchunguzi ungali unaendelea ili kubaini ni kwa nini ndege hiyo ilichepuka kutoka katika mkondo wa safari yake.
Pamoja na ukweli kuwa nchi kadhaa zinahusika katika juhudi za kuitafuta kwa kutumia teknolojia ya kisasa, bado haijatangazwa kama ndege hiyo iliyotegenezwa Marekani imepata athari gani.
CHANZO: MWANANCHI