Polisi mjini Mombasa
Polisi mjini Mombasa wamemkamata mshukiwa wa tatu wa ugaidi na kunasa silaha zaidi katika gari lililokuwa limebeba mabomu mawili Jumatatu jioni katika mtaa wa Changamwe.
Mshukiwa huyo alikamatwa na polisi wa kupambana na ugaidi waliopata taarifa kutoka katika idara ya ujasusi na mashirika mengine ya usalama.
Inaaminika kuwa mshukiwa huyo alikuwa kiongozi wa njama ya shambulizi iliyotibuka na alikuwa ametoroka wakati washukiwa wenzake wawili walipokamatwa Jumatatu jioni.
Washukiwa waliokamatwa Jumatatu walikuwa wanapanga kufanya mashambulizi katika sehemu ambazo hawakutaja mjini Mombasa.
Walitarajiwa kufikishwa mahakamani Jumanne ingawa polisi waliomba muda zaidi kufanya uchunguzi.
Kwa mujibu wa kamishna mkuu wa Mombasa, wataalamu wa mabomu walitegua mabomu hayo.
Pia walinasa mitungi sita yenye uzito wa kilo 60 yenye uwezo wa kulipua majengo, maguruneti sita, bunduki aina ya AK-47 na risasi 270 pamoja na vifaa vitano vya kulipua mabomu ikiwemo simu ya mkononi.
Maafisa wa ujasusi waliweza kunasa mawasiliano yao na kuweza kuwakamata washukiwa hao.
Mombasa ni mji unaosifika kwa utalii lakini hivi karibuni umekuwa ukikumbwa na harakati za vijana wa kiisilamu kukumbatia itikadi kali za kidini.