BASI LAUA WATU 19 WAKIMSITIRI MAREHEMU



WATU 19 wamekufa papo hapo wakiwemo askari Polisi wanne katika ajali ya barabarani, wakati basi linalomilikiwa na Kampuni ya Sumry, lilipopamia watu hao wakati wakimsitiri mtembea kwa miguu, aliyekufa kwa kugongwa na gari lisilofahamika.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana katika Kijiji cha Utaho, kilometa 20 nje ya Mji wa Singida katika Barabara Kuu ya Singida Dodoma.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Kamishina Msaidizi Mwandamizi, Geofrey Kamwela, alisema jana kuwa mbali na askari hao, wengine waliokufa papo hapo ni viongozi watatu wa kijiji hicho na wananchi wanaowaongoza na wengine wanne ambao hawajatambulika.

Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, askari waliokufa katika ajali hiyo ni Koplo Boniface Magubika, PC Jumanne Mwakihaba, PC Novatus Tarimo na PC Michael Mwakihaba na wote wanatoka katika kituo kimoja cha kazi.

Viongozi wa Kitongoji na Kijiji cha Utaho waliokufa ni Ramadhan Mjengi, ambaye ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Paul Hamis, ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji na Ernest Salanga ambaye ni Mwenyekiti Kitongoji.

Wananchi wanaowaongoza katika kijiji hicho waliokufa ni Saidi Rajabu, Ushirika Itambu, Chima Mughenyi, Salim Juma, Abeid Ramadhan, Mwinyi Hamis na Issaha Hussein.

Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, miili ya watu wengine wanne haikuwa rahisi kutambulika mara moja na wote wamehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa mjini Singida.

Kamanda Kamwela alisema ajali hiyo ilisababishwa na basi la abiria lenye usajili namba T.799 BET aina ya Nissan, mali ya Kampuni hiyo ya Sumry, inayomilikiwa na Mohamed Abdallah wa Sumbawanga, lililokuwa likienda jijini Dar es Salaam likitokea Kigoma.

Alisema kuwa basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Paul Njilo, mkazi wa Dar es Salaam, liliwagonga waenda kwa miguu hao waliokuwa wamekusanyika kando ya barabara wakisaidiana na askari Polisi kuondoa mwili wa marehemu Gerald Zephania, aliyekuwa amegongwa na lori lisilofahamika juzi saa moja usiku.

Katika ajali hiyo kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, watu wengine wanane walijeruhiwa na wamelazwa katika Hospitali ya Misheni Puma ya mjini Singida.

Habari kutoka eneo la tukio zinasema kilichosababisha ajali hiyo huenda ni kuegeshwa vibaya kwa gari la Polisi, wakati likipakia mwili wa marehemu Gerald, aliyekuwa amegongwa na lori mapema kabla ya basi hilo kufika hapo. Inadaiwa gari la Polisi liliziba barabara.

Akizungumzia ajali hiyo katika Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam jana, Kamishna Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, alitoa pole kwa wananchi wote waliofiwa na ndugu zao na kuwaombea majeruhi kupona haraka.

Alisema Askari wa Usalama Barabarani hawatakuwa na muhali na dereva yeyote atakayekwenda kinyume na Sheria ya Usalama Barabarani. Kutokana na hilo, ametoa mwito kwa madereva kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarni, ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

“Polisi iko imara kuchukua hatua zozote za kisheria, kwani kuna baadhi ya watoa huduma wa usafiri hugoma pale wanapotaka kuchukuliwa hatua kwa sababu mbalimbali matokeo yake ni uvunjaji wa sheria kwa makusudi,” alisema.

Alisema Jeshi la Polisi limeanzisha msako mkali wa dereva wa basi hilo ambaye alitoroka ili kufikishwa mahakamani, na kuwaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahalifu wa aina yeyote ile, ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani. Imeandikwa na Abby Nkungu, Singida na Theopista Nsanzugwanko, Dar (CHANZO: HABARILEO)
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company