Dar yapendekeza wilaya mbili mpya

www.hakileo.blogspot.com
Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam umependekeza kuongeza idadi ya wilaya zake kutoka tatu hadi tano, katika bajeti ya mwaka huu wa fedha inayotarajiwa kusomwa katika Bunge lijalo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki baada ya kikao cha Kamati ya Ushauri wa Mkoa (RCC), kilichofanyika juzi. Sadick alisema ombi hilo limetolewa baada ya kujadili mapendekezo ya wabunge wa mkoa huo katika vikao vya mabaraza ya madiwani katika wilaya husika.

“Timu ya wataalamu kutoka halmashauri zote tatu, jiji pamoja na sekretarieti ya mkoa iliundwa na kupewa jukumu la kuandaa mapendekezo na kufanya mgawanyo wa wilaya kulingana na vigezo husika,” alisema Sadick na kuongeza kuwa hilo litakwenda sambamba na uongezaji wa kata na mitaa kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Mabadiliko hayo yakiridhiwa, mkoa utakuwa na Wilaya za Ilala, Kinondoni, Temeke, Kigamboni na Ubungo. Pamoja na wilaya hizo kutakuwa na jimbo jingine katika wilaya mpya ya Kigamboni.

Mabadiliko mengine yaliyopendekezwa ni ongezeko la kata na mitaa ili kurahisisha ufikishaji wa huduma kwa wananchi. Mkoa umekusudia kuongeza idadi hiyo kutoka kata 90 zilizopo sasa mpaka 113 na mitaa itakayofikia 570.

“Mapendekezo yaliyotolewa yanataka kuwepo kata 37 katika Manispaa ya Ilala badala ya 26 zilizopo na Temeke iwe na kata 42 badala ya 30 zilizopo. Manispaa ya Kinondoni itabakiwa na kata zake 34.”
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company