Ibada hiyo ambayo itafanyika saa 7 mchana katika kanisa lililopo ndani ya maeneo ya Bunge, itaendeshwa na Askofu wa Jimbo la Dodoma, Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga.
Kuendeshwa kwa ibada hiyo maalumu, kulitangazwa bungeni mjini Dodoma jana na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samiah Suluhu Hassan.
“Atakuja kusali katika kanisa la hapa bungeni saa 7 mchana kwa lengo la kuliombea Bunge Maalumu…Wakristo wote tunaombwa kujumuika katika sala hii,” alisema.
Ibada hiyo inaendeshwa zikiwa zimepita siku chache tu baada ya Maaskofu 32 wa kanisa hilo kutoa waraka maalumu wa Pasaka kwa wajumbe wa Bunge hilo wakiwataka kuheshimu maoni ya wananchi.
Maaskofu hao walisema ili kupata Katiba bora, wajumbe wanapaswa kuheshimu kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuitumia kama ilivyokusudiwa na sheria.
CHANZO MWANANCHI