*MEMBE KUFUNGUA MKUTANO WA KIMATAIFA JUU YA UALBINO.


Frank Mvungi- Maelezo
WAZIRI wa wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe anatarajiwa kuwa mgeni rasmi mkutano wa Kimataifa wa Ualbino utakaofanyika mwezi Mei mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Afisa Mahusiano na habari wa Chama cha Albino Tanzania (TAS), Josephat Torner wakati wa mkutano na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam.
Torner alisema mkutano huo wa siku moja utafanyika katika hoteli ya Serena Jijini Dar es salaam na utawahusisha washiriki toka mataifa mbalimbali yakiwemo Nchi za Afrika Mashariki, Marekani, Nchi za Ulaya na Nchi za Kusini mwa Afrika.
Alisema moja ya matarajio ya mkutano huo ni kupata sauti ya pana ya Kimataifa kuutaka Umoja wa Mataifa kuitangaza tarehe 4 mwezi Mei kuwa Siku ya Kimataifa ya Ualbino.
Aliongeza kuwa lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kutafakari vikwazo vinavyosababisha tofauti ya umri wa kuishi kati ya watu wenye ulemavu na watu wengine.
“Hii inatokana na ukweli kwamba kwa Tanzania wastani wa umri wa kuishi kwa watu wenye ualibino ni miaka 30 wakati kwa watu wengine ni miaka 60”2, alisema Torner.
Alisema sababu zinazochangia watu wenye ulemavu wa ualbino kuishi nusu ya umri wa Watanzania wengine ni kukabiliwa na saratani ya ngozi.
Alitoa wito kwa watu wote wenye ualbino,wazazi,walezi na wadau mbalimbali na umma kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho haya.
Maadhimisho ya Siku ya Albino yalianzishwa hapa nchini mwaka 2006 na tangu mwaka huo yamekuwa yakileta hamasa katika nchi mbalimbali Duniani.

Kilele cha maadhimisho hayo hapa nchini kinatarajiwa kuwa siku ya tarehe 4/5/2014 na kauli mbiu ikiwa ni Haki ya Afya,Haki ya Uhai.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company