Uchunguzi wa maoni uliofanyika nchini Afrika Kusini unaonyesha kuwa, chama tawala cha African National Congress ANC kwa mara nyingine tena kitajipatia ushindi kwenye uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika kesho kutwa Jumatano nchini humo. Uchunguzi huo wa maoni unaonyesha kuwa, chama cha ANC kitajipatia ushindi wa zaidi ya asilimia sitini ya kura zitakazohesabiwa. Uchunguzi huo wa maoni unaonyesha kuwa, chama cha Muungano wa Demokrasia, chama kikuu cha upinzani nchini humo, kinaweza kujipatia karibu asilimia 20, kiwango ambacho kinaonekana kuwa kikubwa kwa chama hicho cha upinzani kikilinganishwa na cha uchaguzi uliofanyika miaka mitano iliyopita. Chama cha ANC kinashikilia uongozi wa nchi hiyo tokea ulipoangushwa utawala wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994. Hivi sasa, chama cha ANC kinakalia viti 264 kati ya viti 400 katika bunge la Afrika Kusini. Kwa mujibu wa katiba ya Afrika Kusini, rais wa nchi hiyo huchaguliwa na wabunge na bila shaka chama kitakachojipatia wingi wa viti ndicho kitakachoongoza serikali ya nchi hiyo.