Bunge la bajeti linaanza kesho huku Serikali ikiwa imetoa mwelekeo wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/15 kuwa ni Sh19.6 trilioni, ikilinganishwa na Sh18.2 za Bajeti iliyopita.
Vipaumbele vya bajeti hiyo ni kuendeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulioanza mwaka 2011 na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao unajumuisha maeneo sita ya kitaifa ya kilimo, elimu, maji, utafutaji wa rasilimali fedha, nishati, uchukuzi na uboreshaji wa mazingira ya kufanyia biashara.
Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, matumizi ya kawaida kwa mwaka ujao wa fedha yanalenga kufanikisha mambo 20 muhimu, yakiwamo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014, Uchaguzi Mkuu 2015, kukamilisha mchakato wa Katiba na nyongeza ya mishahara na kulipa kwa wakati.
Waziri huyo alisema makadirio ya matumizi ya maendeleo ni Sh7.7 trilioni sawa na asilimia 39 ya matumizi yote ya Serikali na kati ya fedha hizo miradi ya maendeleo imetengewa Sh5.4 trilioni sawa na asilimia 27 na matumizi mengine ya maendeleo ni Sh2.2 trilioni.
Pia alisema katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali imekusudia kukopa Sh4.2 trilioni kutoka vyanzo vya mapato vya ndani na nje ili kuziba pengo la mapato.
Serikali imetenga Sh5.4 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na imeonyesha vipaumbele vyake vikuu katika miradi hiyo ya maendeleo ni kilimo, elimu, maji, utafutaji wa rasilimali fedha, nishati, uchukuzi na uboreshaji wa mazingira ya kufanyia biashara huku michezo ikikosekana katika vipaumbele hivyo.
Sisi tunaamini sekta ya michezo ilistahili kuingizwa katika vipaumbele vya Serikali katika bajeti yake ya 2014/15 kwani sekta hii ikitengewa fedha nyingi na kuwekewa misingi imara ni chanzo kikubwa cha mapato.
Tumeshuhudia katika nchi mbalimbali duniani ambazo Serikali zao zinaithamini sekta ya michezo kwa kuitengea bajeti kubwa ya miradi ya maendeleo, wanamichezo wa nchi hizo wamekuwa wakinufaika na kupata mapato makubwa na hivyo kulipa kodi kubwa ambazo zimekuwa ni chanzo kikubwa cha mapato.
Ni wazi ukiangalia kwa undani nchi zote zilizoendelea katika michezo utaona kwa nanma moja au nyingine kuna nguvu nyingi za Serikali za nchi hizo hasa utagundua Serikali za nchi zao hutoa fedha na kuboresha miundombinu ya michezo ili kuweza kuwa na programu nzuri za kuendeleza michezo na husaidia timu zao za taifa.
Tunaamini kwamba hata kama mapato ya nchi ni madogo, Serikali ikiwa na dhamira ya dhati ya kupenda michezo na kuipa kipaumbele, haitashindwa kupata vyanzo mbalimbali vya mapato kwa ajili ya kuhakikisha sekta ya michezo inakuwa katika vipaumbele vya bajeti na kutengewa fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Inaeleweka kuwa Tanzania tuna bahati ya pekee duniani kwani tuna utajiri mkubwa wa rasilimali ambazo kama kama zitatumika ipasavyo zitanufaisha sana taifa letu na wanamichezo wetu watapata vifaa vya michezo kwa bei nafuu, viwanja vya michezo na walimu bora wa michezo.
Hata hivyo katika hali ya kushangaza utajiri huo wa rasilimali umekuwa ukionekana kunufaisha wachache huku hali hiyo ikionekana kama ni jambo la kawaida. Tunatarajia wabunge watatuunga mkono na kuisimamia Serikali ipasavyo katika kuhakikisha kuanzia Bunge hili la bajeti sekta ya michezo inatambuliwa na kutengewa fedha nyingi katika miradi ya maendeleo.(CHANZO: MWANANCHI)