Jenerali Mwamunyange:Hatuhusiki na siasa katu


NA JOHN NGUNGE

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, amekwepa kuzungumzia au kutoa ufafanuzi kuhusu kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi kuwa iwapo muundo wa serikali tatu utapitishwa katika katiba mpya, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linaweza kupindua nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano mkuu wa nane wa Wakuu wa Idara za Ukaguzi za Majeshi (DIWG) kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo za Kusini mwa Afrika (SADC), Jenerali Mwamunyange, alisema hawezi kujiingiza katika masuala ya siasa.

Alitoa jibu hilo kufuatia swali la mwandishi wa NIPASHE aliyetaka kujua (CDF) anatoa kauli gani kufuatia baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini kulihusisha jeshi hilo na siasa huku wakidai iwapo muundo wa serikali tatu ambao unalitikisa Bunge Maalum la Katiba utapita, basi, jeshi linaweza kupindua nchi.

“Siwezi kujibu hilo swali, siwezi kujiingiza katika siasa. Ni sawa kama mimi mchezaji wa mpira wa miguu uniulize swali kuhusu mpira wa tennis,” alisema Jenerali Mwamunyange.

Baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitoa kauli ndani na nje ya Bunge Maalum la Katiba kwamba ikiwa muundo wa serikali tatu utapitishwa kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jeshi linaweza kuasi na kupindua nchi ikiwa serikali ya Muungano itakosa mapato na kushindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.

Mara ya kwanza Rais Jakaya Kikwete akizindua Bunge Maalum la Katiba alitoa kauli hiyo, akionya kuwa kuanzishwa kwa muundo wa serikali tatu kunaweza kuwa na madhara mengi kijamii, kutokana na gharama za kuziendesha.

Alisema serikali tatu zinazoundwa ikiwamo za nchi washirika kwa maana ya Zanzibar na Tanganyika kutaifanya ile ya Muungano kutokuwa na nguvu ya kujiendesha kwa sababu ya kutokuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato, hivyo kutishia uimara wake.

Ni kutokana na hali hiyo, Rais alisema kwa sababu suala la ulinzi ni Muungano serikali husika inaweza kushindwa kulipa hata mishahara ya wanajeshi na kuwa chanzo cha kupindua nchi.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, katika kanisa la Methodist mjini Dodoma Aprili 13, mwaka huu wakati wa kumsimika Askofu Joseph Bundara, alikoleza kauli hiyo.

Kauli hiyo ililalamikiwa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwa Lukuvi alikuwa anatoa vitisho ili wananchi waogope kuunga mkono muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Kauli ya Lukuvi ni moja ya sababu zilizowalazimisha Ukawa kususia Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu.

Jaji Warioba kwa upande wake amesema kwamba kwa jinsi anavyoifahamu JWTZ tangu akiwa kiongozi mwandamizi wa serikali, kimaadili hawawezi kusukumwa na mundo wa serikali tatu kupindua nchi.

Alisema kwamba wanajeshi kwa muda mrefu wakekuwa wavumilivu na kwamba tatizo walilonalo ni kupiga mizinga 21 Dar es Salaam na Zanzibar katika nchi moja kana kwamba kuna zaidi ya amiri jeshi mkuu zaidi ya mmoja.

KUWENI TAYARI WAKATI WOTE
Mapema akifungua mkutano huo jijini hapa jana, Jenerali Mwamunyange, aliwataka wakuu wa idara za ukaguzi katika majeshi ya SADC, kuhakikisha majeshi yao yanakuwa tayari wakati wowote kutekeleza majukumu yao.

Alisema ukaguzi wa majeshi ni jambo muhimu ili kujua iwapo yapo tayari kutekeleza majukumu yao katika kulinda amani, usalama wa mipaka ya nchi wanawachama.Alisema suala la majeshi kuwa tayari ni muhimu sana katika ukanda huo.

“Suala la majeshi kuwa tayari, likiwa na vifaa ni jambo muhimu sana katika ukanda wetu kwa sasa kwa sababu ya kuwapo kwa hali isiyotabirika kiusalama.

“Hali hii inataka ukanda wetu kujiweka tayari muda wote kukabiliana na matukio,” alisema.

Aliwataka wakuu hao kuwa makini na suala la ukaguzi ili DIWG, ambacho ni macho, masikio na vidole vya Wakuu wa Majeshi wa nchi wanachama kiweze kufanya kazi na kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

CHANGAMOTO
Akizungumzia changamoto ya chombo hicho, Jenerali Mwamunyange, alisema ukaguzi wa majeshi una gharama kubwa kwani vikao kuhusiana na jambo hilo vinafanyika mara kwa mara hivyo kuwasafirisha watu kunahitaji fedha.

Alisema tofauti za taratibu za kimajeshi kuwa ni changamoto nyingine.

Hata hivyo, alisema Tanzania inanufaika na uwapo kwa chombo hicho ambapo kwa mambo mengine wanabadilishana mawazo, uamuzi na utekelezaji wa majukumu mbalimbali wanayokubaliana na wenzao.

Katika mkutano huo, Tanzania inakuwa mwenyekiti wa DIWG chini ya Brigedia Jenerali Emmanuel Edward Maganga.

Brigedia Jenerali Maganga, alisema watatekeleza vizuri jukumu la kukagua mafunzo, utendaji na vifaa na kisha kutoa taarifa kwa wakuu wa majeshi ambao nao hutoa taarifa kwa wakuu wa nchi.

Naye mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Brigedia Jenerali Bornwell Njilika kutoka Zambia alisema katika kipindi cha uongozi wake wamefanikiwa kufanya ukaguzi wa majeshi licha ya kukabiliwa na changamoto ya kifedha na kimawasiliano na sekretarieti ambayo ilikuwa Botswana.
CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company