Kilosa walia na DED Hospitali ya Wilaya kukosa dawa,vifaa


Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid
Wananchi katika baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, wamemlalamikia Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo (DED), Masalu Mayaya, kwa madai ya kutotekeleza wajibu wake katika kusimamia maendeleo ya sekta ya afya.

Wananchi hao wametoa malalamiko hayo kufuatia kuwapo kwa madai kwamba Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, imetelekezwa na hivyo kukosekana kwa huduma muhimu vikiwamo vifaa tiba na dawa.

Wananchi hao walisema madai ya kukosekana kwa huduma bora za afya katika hospitali hiyo ya wilaya kumesababishwa na Mkurugenzi huyo kutokemea matumizi mabaya ya fedha zinazotengwa na serikali.

Hata hivyo, Mayaya alipoulizwa kuhusu madai ya wananchi hao, alisema tayari ofisi yake imeanza kufuatilia maagizo ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Ameir Mbaraka, kuhusu fedha za miradi ya jamii zilizotengwa mwaka jana.

“Sioni kwa nini nalaumiwa na kupigiwa kelele kama niliyefanya uhalifu, badala yake wananchi walipaswa kuzingatia ukweli kwamba huduma za afya katika hospitali ya wilaya, ni changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi, lakini hakuna matatizo makubwa kiasi hicho,” alisema Mayaya.

Aliongeza kuwa jamii inapaswa kutambua majukumu ya halmashauri pamoja na kuacha tabia ya kuwaingiza watendaji katika tuhuma za ubadhirifu ama ufisadi, badala yake wawe na subira kuona jinsi wanavyoshughulikia matatizo yanayoikabili sekta hiyo pamoja na kuyapatia majibu madai ya huduma duni kwa jamii.

Baadhi ya wananchi hao walidai kwamba huduma duni katika hospitali yao ya wilaya, zimechafua hali ya hewa na kupunguza kasi ya moyo ya wananchi kujitolea katika masuala ya kijamii.

“Tumekuwa tukilazimika kutafuta huduma hizo kwenye maeneo nje ya wilaya yetu ya Kilosa, lakini badala yake wananchi wamekuwa wakihangaika huku na kule kwa ajili ya kupata huduma hizo ambazo ni haki ya msingi ya maisha yao ya kawaida,” alisema Dickson Kawindwa.

Kawindwa, mkazi wa mjini Kilosa na mratibu wa asasi isiyo ya kiserikali na inayojihusisha na ufuatiliaji wa mambo ya kijamii katika masuala ya afya, alisema halmashauri imeonekana kushindwa kuwajibika kwenye sekta hiyo na hivyo kuibua malalamiko ya wananchi.

Mariam Himba na Husna Mohammed, wakazi wa vijiji vya Msowero na Mvumi, walisema kwa nyakati tofauti kwamba ukosefu wa vitendea kazi na dawa muhimu kwenye hospitali hiyo, ni ya madiwani kupoteza thamani ya wananchi.

“Jamii inajiuliza kama hospitali ya wilaya iko katika hali mbaya kiasi hicho, je; vituo vya afya vijijini vina hali gani?," Alihoji.

Himba alisema kwa msingi huo wananchi watalazimika kurejea katika maisha ya ujima ya kutegemea tiba na dawa za asili pamoja na huduma za tiba za waganga wa kienyeji.

Wananchi hao walimtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, kufanyia kazi tatizo la kukosekana kwa huduma bora na makini wilayani humo.

Aidha, kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, aliwaahidi wananchi hao kwamba atafuatilia hali hiyo.
CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company