Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Abdallah Bimani.PICHA|MAKTABA Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Zanzibar. Chama cha Wananchi (CUF) kimesema wanasiasa wanaojadili suala la kuendelea au kutokuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), wanastahili kujiuzulu au kufukuzwa ndani ya vyama vyao.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Salmin Awadh Salmin kusema kuwa Wawakilishi wa CCM wanajiandaa kuwasilisha hoja binafsi kwenye Baraza hilo ili kuwapa nafasi wananchi waulizwe iwapo wanataka kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa au vinginevyo.
Salmin aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Kibandamaiti, Unguja kwa kuwa wanaona kwamba lengo la kuundwa kwake halina dalili njema kwa siku za usoni.
Jana, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Abdallah Bimani alisema: “Kimsingi mpango huo unakwenda kinyume na uamuzi wa vyama vya CCM na CUF ambao ulipitishwa na kuridhiwa na vikao vya juu vya vyama hivyo viongozi wanaopinga jambo hilo wanaonyesha kupingana na uamuzi wa vyama vyao.”
Ajenda ya siri
Mkurugenzi huyo wa CUF alikana chama chake kuwa na ajenda ya siri ya kuvunja Muungano au kuyasambaratisha Mapinduzi ya Zanzibar na kusema kinachopiganiwa ni muungano wenye usawa, haki na heshima kila upande wa washirika.
Kuhusu Ukawa kususia Bunge Maalumu la Katiba, Bimani alisema chama chake kimetoa masharti matatu yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya kubadilisha msimamo wake. Alitaja masharti hayo kuwa ni kuijadili Rasimu ya Katiba kama iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba; wajumbe wa CCM kuacha matusi, vijembe na ubaguzi na hilo lithibitishwe kwa maandishi na viongozi wake wa kitaifa.
Jambo la tatu ni kuhakikishiwa kuwa vikao vya Bunge vitumike kujadili rasimu na si sera za vyama vya siasa kwa vile ndiyo mwanzo wa kukaribisha malumbano na kusababisha Bunge kupoteza mwelekeo na kuweka nyufa katika Umoja wa Kitaifa.
Mbatia alaani
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia amelaani kauli zilizotolewa na viongozi wa CCM katika mikutano yake ya Unguja na Pemba.
Mbatia alisema kuwa hoja ya CCM kutaka kufuta Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar inapaswa kulaaniwa kwani italeta machafuko. “Serikali ya Umoja wa Kitaifa si ya CCM na CUF tu, ni ya wananchi wote, ni makosa makubwa kudhani kuwa Serikali hiyo ni ya vyama hivyo viwili. Ilifanyika hivyo ili kutokuendelea umwagaji damu,” alisema Mbatia.
Mbatia alisema madai ya CCM kuwa Maalim Seif hatalipwa mafao yake hayana msingi wowote kwa sababu anacholipwa ni haki yake. “Kwani hayo mafao ni ya CCM au wanaolipa kodi ni CCM tu? Ukweli ni chanzo cha amani na haki ni msingi wa amani, ukweli utatuweka huru.”
Aliitaka CCM kutokuwaingiza Watanzania katika machafuko kwa sababu tu ya uroho wa madaraka, badala yake kijenge hoja za msingi katika majadiliano ya Katiba badala ya kuwatisha watu kwa udini, jeshi na kuvunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa.