Sudan Kusini yatumbukia kwenye mapigano na majanga mbalimbali

CHANZO http://kiswahili.irib.ir/
kikabiliwa na migogoro kadhaa katika siku za hivi karibuni. Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, mauaji, ukame, baa la njaa na hata maelfu ya wananchi wa nchi hiyo kuwa wakimbizi ni miongoni mwa matukio machungu yanayoikumba nchi hiyo siku baada ya siku. Hivi karibuni, Umoja wa Mataifa umefichua tukio jingine la kuwepo wanajeshi watoto kwenye safu ya medani za mapigano nchini humo. Navy Pillay, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa, zaidi ya watoto elfu tisa wanatumikishwa kwenye mapigano ya ndani nchini humo. Pillay ameongeza kuwa, majeshi ya serikali ya Sudan Kusini pamoja na waasi wanaoongozwa na Riek Machar makamu wa zamani wa rais, wamekuwa wakiwatumia watoto kama askari wao kwenye vita hivyo vilivyodumu kwa miezi minne sasa. Ukweli huo mchungu umefichuliwa katika hali ambayo, kila siku wananchi wengi wasio na hatia wamekuwa wahanga wa vita vya kugombania madaraka nchini humo. Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mwendelezo wa wimbi la mapigano nchini Sudan Kusini umesababisha pia kuwepo kwa vitendo vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu, mauaji ya raia wasio na hatia na kutiwa watu mbaroni kiholela. Kabla ya hapo, ujumbe maalumu wa kutafuta amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ulitangaza kuwa, vimepatikana viwiliwili kadhaa vya raia na askari waliotiwa mbaroni huko Juba, mji mkuu wa nchi hiyo na katika majimbo ya Upper Nile na Jonglei. Hivi karibuni viongozi wa Umoja wa Mataifa waliwatuhumu viongozi wa serikali ya Juba na waasi kwa kutozingatia mustakbali wa nchi hiyo. Viongozi hao wamesisitiza kuwa, Sudan Kusini inakaribia kutumbukia kwenye lindi la maafa na majanga makubwa. Kwani shughuli za kilimo zimesimama kikamilifu kutokana na kuendelea mapigano nchini humo. Taarifa zinasema kuwa, ukame ni janga jingine linaloinyemelea kwa kasi Sudan Kusini, suala ambalo limewatia hofu kubwa viongozi wa Umoja wa Mataifa. Hayo yote yanajiri katika hali ambayo, maelfu ya raia wa nchi hiyo wanapewa hifadhi ya ukimbizi kwenye kambi za umoja huo ndani ya ardhi ya nchi hiyo. Hata hivyo, wakimbizi hao hawako salama, kwani bado wanakabiliwa na mashambulio ya mara kwa mara ya makundi yanayopambana nchini humo. Wiki za hivi karibuni, makumi ya wakimbizi waliopewa hifadhi kwenye kambi ya Umoja wa Mataifa kwenye mji wa Jonglei waliuawa na kujeruhiwa, natija ya mapigano yanayoendelea kati ya makundi hasimu nchini Sudan Kusini. Kambi hiyo inawahifadhi wakimbizi wa kabila la Nuer, ambalo ni kabila la Riek Machar kiongozi wa waasi nchini humo. Kabla ya hapo, waasi wanaofungamana na Machar waliushambulia mji wenye utajiri wa mafuta wa Bentiu ulioko katika jimbo la Unity na kuwauwa kwa halaiki mamia ya raia wa kabila la Dinka, kabila analotoka Rais Rais Salva Kiir wa nchi hiyo. Hayo yanajiri katika hali ambayo, kushadidi mapigano na machafuko kutaivuruga zaidi nchi hiyo, ambapo Marekani na Ufaransa zimesisitiza juu ya kuwekewa vikwazo Sudan Kusini ikiwa ni njia ya kuishikisha adabu nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company