CHANZO http://kiswahili.irib.ir/
Jumuiya ya Afrika Mashariki imetoa wito kwa viongozi wa nchi 5 wanachama kuwahusisha wananchi wao katika masuala yanayohusiana na utangamano kwenye jumuiya hiyo. Akisoma taarifa ya mwisho ya kikao cha 12 cha wakuu wa nchi na serikali wa jumuiya hiyo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema wananchi wasipohusishwa kwenye mchakato wa kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, itakuwa vigumu kwa mikakati iliyowekwa kufanikiwa. Rais Kenyatta ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa EAC amesema miongoni mwa mambo yaliyokubaliwa kwenye mkutano huo uliofanyika mjini Arusha, Tanzania, ni pamoja na kuharakishwa mchakato wa kubuni sarafu moja ya Afrika Mashariki. Kuhusiana na hilo Rais Kenyatta amesema kuweko sarafu moja kutaharakisha ukuaji wa uchumi katika nchi 5 wanachama. Mbali na Rais Kenyatta, viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na marais Yoweri Museveni wa Uganda na Jakaya Kikwete wa Tanzania. Rwanda iliwakilishwa na Waziri Mkuu wake, Pierre Damien Habumuremyi nayo Burundi ikawakilishwa na Makamu wa kwanza wa rais, Prosper Bazombanza