WAJAWAZITO WALALAMIKIA ‘RUSHWA’ KITUO CHA AFYA SIMAMBWE

Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Simambwe, Salome Mwaipopo (kulia) akizungumza na mwandishi wa habari hizi. Kushoto ni mmoja wa manesi wa kituo.

Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Simambwe, Salome Mwaipopo (kulia) akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Sehemu ya jengo la Kituo cha Afya Simambwe, likitoa huduma.
====== ====== ======
Wajawazito walalamikia ‘Rushwa’ Kituo cha Afya Simambwe
Mbeya Vijijini

BAADHI ya akinamama na wanakijiji wa baadhi ya vijiji vya Kata ya Tembela Wilaya ya Mbeya Vijijini wamewalalamikia wauguzi na wahudumu wa afya katika Kituo cha Afya Simambwe kwa kile baadhi yao kuwaomba kitu kidogo (rushwa) hasa kwa wajawazito wanapofika katika kituo hicho kupata huduma.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanawake kutoka vijiji vinavyohudumiwa na kituo hicho vya Usoha Njiapanda, Shibolya, Simambwe, Garijembe, Ilembo Usafwa, Ngoha na Zunya walisema mjamzito amekuwa akiombwa kutoa shilingi 2000 kila anapojifungulia nyumbani kwa dharura baada ya kushindwa kufika katika kituo hicho.


Mmoja wa akinamama aliyezungumza na mwandishi wa habari hizi ambaye aliomba kutotajwa kwa kuwa huenda akapata taabu kihuduma za afya kituoni hapo, alisema kwa sasa ni jambo la kawaida wahudumu kuwaomba chochote wajawazito kituoni hapo.


“…Unajua vijiji vingi vinavyohudumiwa na kituo hiki vipo mbali na miundombinu ya barabara si mizuri, yaani hakuna usafiri zaidi ya bodaboda ambazo lazima zitoke Simambwe…sasa kutokana na hali hii inatokea mjamzito anajifungulia nyumbani kwa msaada wa wakunga wa jadi, akipeleka mtoto huyo kituo cha afya basi wanamuomba shilingi 2000 haijulikani ya nini, sasa hili si tunaamini sio haki,” alisema mama huyo.


Aidha baadhi ya wanakijiji walikilalamikia kituo hicho kwa kitendo cha kulalamika muda wote hakina dawa huku wahudumu wakiwaelekezwa kwenda kununua dawa jambo ambalo wanahisi kuna mchezo mbaya unafanywa na wahudumu hao.


“Muda wote ukienda kutibiwa utasikia kauli za hakuna dawa tunakuandikia nenda kanunue, tena wengine wanaelekeza hadi maduka ya kununua dawa hizo ndio maana baadhi yetu tunahisi kuna mchezo mbaya (kuhujumu dawa) unaofanywa na baadhi ya wahudumu.,” alisema Mzee aliyejitambulisha kwa jina la Kalamwa.


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Simambwe, Salome Mwaipopo alipinga vikali uwepo wa vitendo vya kuomba rushwa kwa watumishi wa kituo hicho na kudai malalamiko kwa wanachi wanaohudumiwa na kituo hicho imekuwa kitu cha kawaida hasa wanapotembelewa na mgeni.


“..Hakuna kitu kama hicho unajua wakazi wengi wa vijiji hivi wamezoea kulalamika hasa wanapotembelewa na mgeni…hakuna wanaoombwa fedha, mjamzito akijifungua nyumbani tunampokea bila masharti na kumpatia huduma anazostahili, si kweli wanachokilalamikia,” alisema Mwaipopo.


Hata hivyo alisema kituo hicho kinahudumia idadi kubwa ya watu zaidi ya uwezo wake jambo ambalo hukifanya kuelemewa kwa idadi ya dawa wanazoletewa, wahudumu na vifaa vingine tiba hivyo kuiomba Serikali kukiongezea mgao wa dawa.


Kituo kinahudumia idadi kubwa ya watu kupita uwezo wake hivyo unakuta hata baadhi ya changamoto kama ufinyu wa dawa na wahudumu vinatokana na hali kama hiyo…,” alisema Mganga huyo Mkuu wa Kituo cha Afya Simambwe. *Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na TGNP
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company