Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akiondoka Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam akiwa kwenye kiti cha magurudumu akisindikizwa na maaskofu wenzake wa kanisa hilo baada ya kuachiwa kwa dhamana jana.
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam akiwa chini ya ulinzi wa polisi, ameachiwa huru kwa dhamana katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, jijini humo.
Kuachiwa kwake kulipokewa kwa nderemo, hoi hoi na vifijo na waumini wake waliojitokeza kwa wingi kumlaki, kiasi cha idadi kubwa ya magari waliyokuwa nayo, kufunga barabara kwa muda wakimsindikiza nyumbani kwake.
Akionekana mnyonge, huku afya yake ikionekana kudhoofu kiasi cha kulazimika kutumia viti maalumu vya wagonjwa, alisogezwa hadi karibu na gari lake aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili lenye namba za usajili T 631 AHD, ambako alisaidiwa kuingia garini.
Kabla ya kupanda gari, Gwajima mwenye kipaji cha kuzungumza, hakuondoka kimyakimya, kwani alisema: ”viongozi wa dini lazima wawe wa kweli na wanapokubaliana jambo, kila mtu anatakiwa aheshimu na atakayekiuka huyo ni msaliti.”
Kabla ya kiongozi huyo kufikishwa kituoni hapo, kulikuwa na taarifa za kufikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, hali ambayo ilisababisha wafuasi wake kufika kwa makundi na kuzunguka maeneo ya kituo hiko.
Askari polisi walitanda kila kona ya kituo hicho, kilichopo eneo la Stesheni na kuzuia watu kupita karibu na eneo la kituo, hali iliyosababisha wafuasi wa Gwajima kukaa mbali kwa hali ya unyonge bila ya kuimba wala kupiga kelele.
Hata hivyo, mara baada ya kutolewa taarifa kuwa kiongozi huyo amepelekwa Oysterbay, wafuasi hao walikodisha magari kadhaa katika kituo cha Stesheni kuelekea huko, wakiungana na wenzao waliokuwa wamefika kituoni hapo tangu asubuhi.
Gwajima alifikishwa kituoni hapo akitokea hospitalini, alipokuwa amelazwa katika hospitali ya TMJ Mikocheni majira ya saa 6 mchana na gari la polisi lenye namba za usajili STL 110 na kuingizwa kituoni moja kwa moja, ambapo waandishi wa habari na wafuasi wake waliamriwa kukaa mbali na eneo la kituo cha polisi.
Wafuasi hao walionekana kukata tamaa kwa kiongozi wao kurudishwa tena kituo cha polisi, ambako huko ndipo alipata matatizo yaliyosababisha kuzimia wakati akihojiwa na makachero wa polisi na kufanya alazwe katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) tangu usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.
Hata hivyo, ilipofika muda wa saa 8 kamili alipata dhamana na kuruhusiwa kuondoka kuelekea nyumbani, akitumia gari lake, Toyota Land Cruiser.
Mara baada ya kuachiwa, waumini wake walipiga kelele huku wakishangilia na kusukuma gari lake wakati likitoka kwenye kituo cha polisi na kumfuata nyumbani kwake.
Safari ya kuelekea nyumbani ilikuwa sio ya kawaida, kutokana na msafara mkubwa wa magari ya waumini wake na kusababisha barabara ya za kuingia na kutoka kituoni hapo, kufungwa kwa muda na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wengine wa barabara.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema Gwajima na wenzake wamepatiwa dhamana kwakuwa makosa yao yanaweza kudhaminika.
Alisema kwa sasa wanaendelea kukamilisha uchunguzi dhidi yao kabla ya kuwafikisha mahakamani kujibu mashitaka yatakayokuwa yanawakabili.
Gwajima alilazwa hospitali ikielezwa hali yake ilibadilika wakati akihojiwa na makachero wa Polisi baada ya kujisalimisha baada ya kutakiwa kufanya hivyo kutokana na kufunguliwa jalada la malalamiko ya kumkashifu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Habari ambazo tovuti hii ilizipata wakati kabla ya kuchapishwa habari hizi zinasema kwamba Gwajima huenda kesho akatakiwa kuripoti tena Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kuendelea na mahojiano.CHANZO: HABARI LEO (Muro)
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago