kiongozi wa kanisa la ufufuo na uzima, Joseph Ngwajima
MAPYA yamezidi kuibuka katika sakata la Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Joseph Gwajima, baada ya kuthibitika kwamba bastola iliyokamatwa katika harakati za kile kinachotajwa kutaka kumtorosha kutoka katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam, ni mali yake.
Aidha, mmoja wa wanafamilia, ameibuka na kuelezea kushangazwa na ujasiri alioupata Askofu Gwajima wa kumtukana Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, na kusema wanafamilia hawako pamoja naye katika hilo, huku wakimtaka amwombe msamaha Askofu Pengo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema jana kuwa uchunguzi wa kina na wa kitaalam, sasa umethibitisha silaha hiyo inamilikiwa kihalali na Askofu Gwajima.
“Kuhusu risasi 17 za short gun ni kwamba Askofu Gwajima anamiliki bunduki aina ya short gun yenye namba 102837 ambayo inatumia risasi za aina ya hizo zilizokamatwa,” alisema Kamanda Kova.
Bastola hiyo ni moja ya vitu walivyokamatwa navyo wafuasi 15 wa Gwajima, wanaodaiwa kula njama za kutaka kumtorosha usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.
Mbali ya bastola hiyo aina ya BERRETA yenye namba CAT5802 iliyokuwa na risasi tatu, risasi 17 za short gun, vingine vilivyokamatwa ni vitabu viwili vya hundi, hati ya kusafiria yenye jina la Gwajima Joseph Mathias yenye namba AB 544809, kitabu cha hundi cha Benki ya Equity, nyaraka mbalimbali za kampuni ya PUMA, chaja ya Simu na Tablets, suti mbili na nguo za ndani.
Aidha, Kova alikanusha taarifa zilizosambaa kwamba polisi wamekwenda nyumbani kwa mke wa Askofu Gwajima kufanya uchunguzi. Alisema taarifa hizo, hazina ukweli wowote.
Alisema mwanamke huyo anajipa wasiwasi bure, kwani hakuna askari yeyote aliyekwenda kufanya upekuzi. Alisema kama wakitaka kufanya hivyo, zipo taratibu za kufuata.
Akijibu swali la waandishi waliotaka kufahamu maswali aliyohojiwa Askofu Gwajima na kusababisha kuzirai, Kova alisema Gwajima ndiye anayeweza kueleza sababu za kuzimia.
Kufikishwa mahakamani
Alisema watu hao watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo mara baada ya uchunguzi kukamilika. Juzi Kamanda Kova alituma taarifa kwa vyombo vya habari za kukamatwa kwa watu 15, waliodaiwa kutaka kumtorosha Gwajima kutoka hospitalini hapo.
Waliokamatwa ni pamoja na wachungaji sita, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU). Watu hao walikamatwa baada ya kudaiwa kutumia nguvu kulazimisha kuingia kumuona askofu huyo, huku wakiwa na begi lililokutwa na vitu mbalimbali, vikiwamo bastola na hati ya kusafiria ya Askofu Gwajima.
Watuhumiwa Waliokamatwa ni Chitama Mwakibambo (32) ambaye ni fundi seremala mkazi wa Gongo la Mboto, Mchungaji Edwin Audex (24), Adam Mwaselele (29) mhandisi na mkazi wa Kawe, Fredrick Fusi (25) mkazi wa Mbezi Beach.
Wengine ni mwanafunzi wa IMTU, Frank Minja (24), Emanuel Ngwela (28), Geofrey William (30) Mhadhiri wa UDSM na mkazi wa Survey, Mchungaji Mathew Nyangusi (62), Boniface Nyakyoma (30), Geofrey Andrew (31), Mchungaji David Mgongolo (24), mfanyabiashara George Msava (45), Mchungaji Nicholaus Patrick (60), George Kiwia (37) na Mchungaji Yekonia Bihagaze (39).
Ndugu aibuka
Katika hatua nyingine, ndugu wa askofu huyo wa Kanisa la Ufufuo na Uzima aliyejitambulisha kwa jina la Methusela Gwajima ameibuka na kulaani hatua ya ndugu yao kumtukana Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Methusela, alisema katika sakata hilo, wanaomba familia isihusishwe na chochote, kwani Mchungaji Gwajima ana taasisi yake ya kidini na si ya familia.
Alisema pia ana falsafa zake za Ufufuo na Uzima, anazoamini na kuzisimamia, hivyo lazima awajibike mwenyewe.
“Unajua huwezi kumkana ndugu yako wa damu, lakini unaweza kumwambia katika hili sikubaliani na wewe. Sasa ibaki kuwa kazi yake ni kusema ndio au hapana,” alisema.
Alisema kwa sasa familia imekuwa ikipata usumbufu mkubwa kwa kitendo hicho kutoka kwa marafiki wa nje na ndani ya nchi, wakihoji alichofanya ndugu yao.
Aliongeza kuwa katika familia wamekua na kufundishwa maadili na heshima ya kuongea na watu waliowazidi kama vile Pengo. “Tunashangaa yeye maneno kama hayo ameyatoa wapi,” alisema.
“Pengo alitoa ushauri wa busara na wa kuigwa kwamba tunapaswa kuwaachia waumini na wananchi wajiamulie wenyewe kuhusu Katiba inayofaa matokeo yake akaishia kutukanwa na kudhalilishwa kama mtoto mdogo,” alisema.
Alisema maagizo ya Mungu yanakataza kumtusi mtu mwingine kwa namna yeyote ile na hakuna dini ama Serikali inayounga mkono. Alisema sio vyema kugeuza nyumba za ibada kuwa sehemu ya kuporomosha lugha chafu, kwani nyumba ya ibada ni ya kuhubiri habari njema na siyo ulingo wa siasa.
Aliongeza kuwa amefurahishwa na polisi kwa hatua za haraka .“Ukifanya mambo yenye tija kwa jamii ni lazima tutakupongeza, lakini ukifanya mambo ya hovyo katika jamii ni lazima sisi tutakuwa wa kwanza kukukataa” alisema Gwajima.
Atoka ICU
Taarifa iliyotolewa na Daktari wake, Fortunatus Mazigo imesema hali ya Gwajima inaendelea vizuri na jana saa 7 mchana, alitolewa kwenye wadi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu na kumpeleka wadi ya wagonjwa wa kawaida.
Hata hivyo, alisema afya yake imeimarika, japokuwa bado hana nguvu za kutembea na hivi sasa anafanya mazoezi madogo, yatakayomsaidia kuimarika taratibu.
Kuhusu tatizo au ugonjwa unaomsumbua, daktari alisema hajaruhusiwa kuzungumzia tatizo na matibabu wanayoendelea kumpatia hadi hapo atakapopata kibali maalumu, kwa kuwa mgonjwa ndiye mwenye mamlaka ya kusema nini kinamsumbua.(MURO) CHANZO HABARI LEO
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago