Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva |
Awali, Watanzania walikuwa waipigie kura Katiba hiyo Aprili 30, mwaka huu.
Lakini jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema hatua hiyo imetokana na kutokamilika kwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Kwa vile kazi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura ni ya msingi kabla ya kupiga kura, na jukumu la kwanza la Tume ni kukamilisha kazi ya kuboresha daftari. Mengine yanafuata baada ya hapo,”alisema.
Aliongeza: “ Kwa vile zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura halijakamilika, Tume haitaweza kuendelea na zoezi la kupiga kura ya maoni kama ilivyotangazwa awali.”
Awali, ilitangazwa baada ya kukamilika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mfumo mpya wa BVR nchini nzima, upigaji kura ungefanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Tume ilianza Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mfumo wa Biometrick Voters Registration (BVR) baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe, Februari 24 mwaka huu.
Alisema muda mwafaka ukifika, Tume itatangaza tarehe mpya ya Kupiga Kura ya Maoni baada ya kushauriana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Akizungumzia vifaa, Jaji Lubuva alisema kuwa serikali imeshalipa dola za Marekani milioni 72 (sawa na Sh bilioni 122.4) kwa ajili ya vifaa hivyo na kuwa vifaa 7,750 vilivyosalia, vitaletwa nchini kwa awamu.
Katika mchakato wa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mfumo mpya wa BVR, Tume ilihitaji vifaa 8,000 na ilianza na vifaa 250 “Nikiri kulikuwepo na ucheleweshaji wa kulipia vifaa vya kuandikisha wapiga kura, lakini sasa Serikali imelipia vyote, na vitaletwa kutoka China kwa awamu, siku chache zijazo tutapokea vifaa 248 na baadaye vifaa 1,600 na vitafika kwa awamu mpaka idadi itakapofikiwa,” alisema.
Alisema kutokana na kuanza kuingia kwa vifaa hivyo, Tume imejipanga kuhakikisha inakamilisha Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa ukamilifu ifikapo Julai mwaka huu.
Aidha, Lubuva alisema kazi ya uandikishaji wapigakura kwa mkoa wa Njombe, unatarajia kukamilika Aprili 18 mwaka huu na kuwa baada ya hapo Tume itakwenda Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mtwara na Lindi.
“Kama ilivyokuwa Njombe, Tume inatarajia mikoa inayofuata itawahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yao na kujiandikisha kwa tarehe zitakazotangazwa kwenye mikoa husika.”
Hata hivyo, Lubuva alisema kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wadau, wanaoona kuwapo kwa foleni ndefu kuwa ni dalili ya ubovu wa mfumo wa BVR, lakini ukweli hali hiyo ndiyo kielelezo cha kukua na kukolea kwa demokrasia nchini.CHANZO: HABARI LEO (Muro)