Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana amefanya ziara ya kutembelea Mahakama ya watoto na Mahabusu ya watoto za Jijini Dar es salaam. Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara hiyo kwa lengo la kuangalia maeneo ambayo yanahitaji maboresho pamoja na kujionea hali halisi ya uendeshaji wa kesi zinazohusu makosa ya wototo na jinsi watoto wanavyohifadhiwa katika Mahabusu hiyo.
Katika ziara hii Mheshimiwa Naibu Waziri aliwasili katika Mahakama ya Watoto iliyopo ndani ya majengo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam saa mbili asubuhi siku ya tarehe 21Aprili 2015. Akiwa katika Mahakama hiyo ya Watoto aliweza kuhudhulia uendeshwaji wa kesi kadhaa ikiwemo usikilizwaji wa kesi tatu zinahusu makosa ya watoto.
Ambapo kesi ya kwanza ilihusu ubakaji wa mtoto wa kiume dhidi ya mtoto wa kike ambapo ilikuwa katika hatua ya kusomewa maelezo ya awali, kesi ya pili pia ilihusu ubakaji ambayo ilikuwa katika hatua ya utetezi wakati katika kesi ya tatu nayo ilihusu ubakaji katika hatua ya kusikiliza ushahidi upande wa mashitaka.
Mheshimiwa Naibu Waziri alifanikiwa pia kufika katika Mahabusu inayotumika kuhifadhi watoto wakati wakisubiri kesi zao kusikilizwa na watoto ambao kesi zao zimeishaisha. Mahabusu hiyo iliyopo Upanga jijini Dare es salaam inashikilia jumla ya watoto 35, wasichana wakiwa ni wanne (4) na wavulana 31 wenye umri kuanzia miaka 11 hadi 17.
Tanzania bara ina mahabusu za watoto sita (6), ambazo zinatumika kama vituo vya maadilisho ya watoto. Mahabusu hizo zipo mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya na Mtwara. Mahabusu hizi zinatumika kuhifadhi watoto kutokana na sababu mbalimbali zinazohusiana na kesi zao. Sababu hizo ni pamoja na mtoto kukosa dhamana au mdhamini, mtoto kutengwa na hivyo kukosa ndugu au jamaa wa karibu wakati kesi yake ikisubiri tarehe husika na aina ya kosa ambalo halina dhamana, kama kesi za mauaji.
Ziara hii ya Mheshimiwa Naibu Waziri iliweza kubaini mambo mengi kuhusiana na masuala ya watoto. Miongoni mwa masuala yaliyobainika ni kwamba, kesi nyingi za watoto zinahusu ulawiti wa watoto wa kiume kwa wenzao wa kiume au wa kike, mauaji na wizi.
Aidha katika kutekeleza haki ya mtoto ya Kusikilizwa Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana alikutana na watoto katika Mahabusu hiyo iliyopo Upanga Jijini Dar es salaam ili kusikiliza maswali, maoni na changamoto zinazowakabili. Watoto hao (majina yanahifadhiwa kwa sababu maalum) walijieleza kwa kina kesi zinazo wakabili na hali waliyonayo katika mahabusu hiyo, ambapo wengi walilalamikia ucheleweshwaji wa kesi zao kwa upande wa Mahakama na Upande wa Jamuhuri ambaye ndiye mshitaki, hali inayowafanya washindwe katika muda kushiriki katika masomo na kuungana na familia zao.
Mheshimiwa Naibu Waziri ameishauri jamii hasa wazazi na walezi kusimamia malezi sahihi ya watoto na kuacha kupuuza mambo yanayohusu malezi na makuzi ya watoto. Akiongea kuhusiana na makosa ya watoto Dkt. Pindi Chana amekemea zaidi suala la wazazi na walezi kuwafundisha watoto mambo ya kikubwa kabla ya umri wao kufika kwa kuwa kesi nyingi zinazo kabili watoto zimeonekana ni za Ubakaji au Ulawiti, Mauaji na wizi kwa kutumia silaha.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago