Nec yatangaza kuwasili BVR 1,600.


NA SALOME KITOMARY
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imesema vifaa vingine vya Biometric Voters Registration (BVR kits) 1,600 kwa ajili ya uandikishaji wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwenye mikoa minne vitawasili wiki hii.

Nec imesema kwamba vifaa hivyo kwa ajili ya mikoa ya Dodoma, Tabora, Mbeya na Katavi, vitawasili kati ya Jumamosi na Jumapili.

Kadhalika, tume hiyo imesema imeandikisha watu zaidi ya 300,080 katika mkoa wa Njombe. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2012 mkoa huo una jumla ya watu wenye sifa ya kupiga kura 392,634.

Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, alisema vifaa vingine 1,600 vimeshawasili na vitaunganishwa na 498 kwa uandikishaji wa mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mtwara na Lindi. Alisema uandikishaji huo utaanza mikoa hiyo minne Aprili 24, mwaka huu.

Alisema BVR zitakazowasili wiki hii zitapelekwa katika mikoa ya Mbeya, Katavi, Dodoma na Tabora na uandikishaji kuanza Mei 2, mwaka huu.

BVR 250 ndizo za kwanza kuwasili na kutumika katika majimbo ya majaribio ya Kawe, Kilombero na Mlele na baadaye kutumika kwenye uandikishaji katika mkoa wa Njombe.

Uandikishaji katika mkoa huo ulianza Februari 23 na kukamilika Jumamosi iliyopita, zikiwa ni siku 69 kwa kuondoa siku za sikukuu na Jumapili.

Baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika uandikishaji huo ni mashine kushindwa kutambua vidole vigumu na kuchukua muda mrefu kuandikisha mtu mmoja. Hata hivyo changamoto hizo zilipatiwa ufumbuzi.

Kuhusu uandikishaji kurudiwa katika kata za Mjimwema na Kifanya zinazolalamikiwa na wadau, alisema hakuna mwananchi aliyejitokeza na kulalamika kutoandikishwa katika uandikishaji uliomalizika Machi 22, mwaka huu.

Mwenyekiti wa TLP Mkoa wa Njombe, Lukule Mponji, alisema kama tume haitarudisha mashine katika kata hizo kwa ajili ya kuandikisha watu waliobaki katika kata hizo mbili itakuwa imehusika kuminya demokrasia kwa wananchi hao.

“Uandikishaji umekuwa mgumu kutokana muda mchache uliokuwa umepangwa hali iliyosababisha watu kutoka kwenye maeneo mengine kwenda kujiandikisha mjini kwa bahati nzuri mimi nakaa mtaa wa polisi nimeona watu wanatoka Makambako na Wanging’ombe kuja kujiandikisha kwa maana hiyo hawa watachagua Rais tu hawatachagua madiwani na wabunge,” alisema Mponji.

Katibu wa CCM Mkoa wa Njombe, Hosea Mpagike alisema uandikishaki umekwenda vizuri, lakini malalamiko huwa hayakosekani na kwamba wananchi wanapaswa kuwajibika katika mambo ya msingi badala ya kusubiri kusukumwa kila wakati.

Hadi sasa Nec imeshapokea vifaa 2,098, huku 5,902 vikisubiriwa na kwa mujibu wa tarifa za tume hiyo, baada ya kumaliza mikoa yote, jiji la Dar es Salaam na Zanzibar yatakuwa maeneo ya mwisho ili vifaa hivyo vitumike.

Mikoa hiyo na idadi ya wapiga kura kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaonyesha mikoa hiyo itakuwa na wapiga kura Iringa (524,390), Lindi (518,296), Mtwara (773,289) na Ruvuma (783,296).

Mingine ni Dodoma (1,095,320), Tabora (1,124,170), Katavi (271,160) na Mbeya (1,477,370).

Jaji Lubuva alisema wanatarajia hadi kufikia Mei vifaa vyote 8,000 vitakuwa vimefika na hivyo uandikishaji kufanyika kwa haraka nchi nzima.

Wadau wa Uchaguzi walipokutana na Nec, Februari 12, mwaka huu, waliilalamikia tume hiyo kushindwa kuweka wazi ratiba, makadirio ya wapiga kura watakaoandikishwa, mzabuni wa vifaa hivyo, nchi vinakotoka, kiasi cha fedha kilichotolewa na serikali,

kampuni inayohusika na kuweka mfumo wa ndani wa mashine hizo.

Aprili 2, mwaka huu, Nec ilitangaza rasmi kushindikana kwa kura ya maoni kwa Katiba pendekezwa iliyopangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu, baada ya kushindwa kuandikisha wapiga kura kama inavyotakiwa.

Nec ilisema uandikishaji utaendelea na kwamba hadi Julai, mwaka huu watakuwa wamemaliza nchi nzima na kwa kushauriana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar watatangaza tarehe ya kura ya maoni.

Uhaba wa BVR unawapa wasiwasi wadau wengi hususani vyama vya siasa kwamba uandikishaji hautakamilika kufikia Julai na kwamba hali hiyo inaweza kusababisha kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Hata hivyo, wiki iliyopita, Nec iliatangaza kwamba hakuna mpango wowote wa kuahirisha uchaguzi mkuu na kusisitiza kuwa utafanyika kama ilivyopangwa.
CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company