Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa umoja huo, Rashidi Salehe alisema wameamua kusitisha kikao hicho cha madereva nchi nzima ili kuwapa mrejesho wa majibu ambao wanadai hawakuridhishwa nao kutoka kwa Naibu Waziri wa kazi yaliyotolewa katika kikao kilichopita.
“Tumeamua kuitisha kikao kitakachofanyika Aprili 29 mwaka huu kuwaeleza wanachama kauli iliyotolewa na Naibu Waziri wa kazi ,”alisema Salehe.
Salehe alisema kuna mkanganyiko wa kauli iliyotolewa na Naibu Waziri wa kazi ambapo alisema suala la wao kurudi kusoma kuwa halipo huku baadhi ya watendaji kudai kuwa liko palepale.
Alitahadharisha kuwa wanapofanya vikao vyao haimaanishi kuwa wanafanya mgomo kwani hawana siku maalumu ya kupumzika kwani wanachama wao ni walio na kazi na wasio na kazi.
“Sisi madereva tuna haki kama raia wengine, je siku tutakapoenda kupiga kura napo tutaambiwa tumegoma?,” alihoji Salehe.
Salehe alisema jamii inapotoshwa kuhusu matukio ya ajali zinazotokea nchini kwa wamiliki wa magari na maaskari wa usalama barabarani kuwasukumia madereva kitu ambacho si kweli.
“Kuna siri kubwa kuhusu ajali zinazotokea nchini hivyo tunataka kumueleza Waziri Mkuu atusaidie,” alisema Salehe.
Salehe aliwasifia madereva wa Tanzania kuwa ni wenye akili kwa kupita sehemu mbalimbali za milima na mabonde.
“Madereva wanafanyiwa majaribio sehemu zisizo na milima wala mabonde lakini wanaendesha katika barabara ambazo zina miinuko na miteremko mikali huu ni uwezo wa juu,” alisema Salehe.
Aidha alisema baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wanamiliki mabasi na malori na pale sheria zinapovunjwa askari wa usalama barabarani anakatazwa kuzikamata.