Ukawa wahofia Uchaguzi Mkuu kuahirishwa


Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akifungua kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho, Dar es Salaam jana. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti, Juma Duni Haji, Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad (wapili kulia) na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui. Picha na Venance Nestory
Na Raymond Kaminyoge na Nuzulack Dausen, Mwananchi
KWA UFUPI
Lakini mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva amesema viongozi wa kisiasa wasiwajaze wananchi hofu isiyo na sababu kwa kuwa ofisi yake imeongezewa uwezo wa kuandikisha wapigakura na hivyo wana uhakika kazi hiyo itakamilika kabla ya Oktoba.

Dar es Salaam. Hofu ya kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu imezidi kutanda baada ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wanaharakati kueleza kuwa kuna dalili ndogo za uchaguzi huo kufanyika Oktoba.


Lakini mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva amesema viongozi wa kisiasa wasiwajaze wananchi hofu isiyo na sababu kwa kuwa ofisi yake imeongezewa uwezo wa kuandikisha wapigakura na hivyo wana uhakika kazi hiyo itakamilika kabla ya Oktoba.


“Vifaa vimeanza kuwasili. Tumeshapata mashine za (Biometric Voters Registration) BVR 248, nyingine 1,600 zinatarajiwa kuwasili wakati wowote kuanzia sasa na Serikali imeshalipia mashine zote,” alisema Jaji Lubuva.


“Kwa hiyo kadri muda unavyokwenda, ndivyo uwezo wetu wa kusajili unavyokuwa mkubwa zaidi na inawezekana tukamaliza kabla ya Julai.”


Kuhusu kusimamia kauli yake kuwa Kura ya Maoni ingefanyika kama ilivyopangwa lakini ikahirishwa baadaye, Jaji Lubuva alisema wasingeweza kuahirisha mapema kabla ya kuona ugumu wa kazi yenyewe.


Lakini viongozi wa vyama vya upinzani wanaona ahadi hizo ni kama ilivyokuwa kabla ya kuahirishwa kwa Kura ya Maoni na kwamba kasi ndogo ya uandikishaji wapigakura inaweza kusababisha Uchaguzi Mkuu kuahirishwa.


Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti Chadema Freeman Mbowe, mwenyekiti wa NLD Emmanuel Makaidi na mkurugenzi wa asasi ya kiraia ya Concern For Development Initiative in Africa (Fordia), Bubelwa Kaiza, wana hofu ya Uchaguzi Mkuu kuweza kufanyika Oktoba.


Alichosema Lipumba

Akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF, Profesa Lipumba alisema vifaa vilivyowasili ni vichache kulinganisha na mahitaji ya Tume.

Kuna giza nene
“Hadi sasa daftari la wapigakura halijakamilika hata katika mkoa mmoja na bado vifaa vingi havijawasili nchini,” alisema Lipumba ambaye alidokeza kuwa suala hilo litakuwa ajenda kwenye kikao hicho cha siku mbili.

Profesa Lipumba alisema walipokwenda Kenya kwa ajili ya ziara ya mafunzo, walielezwa na Tume ya Uchaguzi ya Kenya kwamba kazi ya uandikishaji wapigakura inatakiwa kuchukua angalau mwaka mmoja.Profesa Lipumba alisema kwa namna ambavyo Jaji Lubuva hayuko huru, Ukawa ina wasiwasi kama mgombea wao wa urais anaweza kutangazwa mshindi iwapo atashinda.

Lipumba alisema NEC waliiomba Serikali BVR 15,000 ili kuandikisha wapigakura kwa urahisi, lakini Serikali ikapunguza na kuidhinisha vifaa 8,000.

Jumla ya wapigakura milioni 24 wanatarajiwa kujitokeza kujiandikisha kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Mbowe ndiye aliyekuwa wa kwanza kueleza hofu hiyo.

Akizungumza na Mwananchi mwishoni mwa wiki, mwenyekiti wa Chadema, Mbowe alisema inaonekana Serikali ya Awamu ya Nne haijajiandaa kuachia madaraka na hivyo kuna uwezekano wa kuomba iongezewe muda.

“Hadi sasa hakuna tunachojua wala kuelezwa. Hofu yetu ni kwamba Serikali inaweza kuomba iongezewe muda kwa kuwa usajili wa wapigakura hautakamilika,” alisema.

“Kama uandikishaji wapigakura wa mwaka 2010 ulifanyika mwaka mmoja kabla, hawa watawezaje kukamilisha katika miezi mitano tu tena kwa kuandikisha kwa BVR?”

Makaidi
Naye Makaidi alisema jana kuwa NEC inachelewesha uandikishaji wa wapigakura kama mbinu ya kuruhusu Serikali iliyopo kuongezewa muda wa kukaa madarakani.

Makaidi, ambaye anadai ameshapitishwa na NLD kugombea urais, alisema haiwezekani vifaa vichelewe kuja nchini wakati kazi ya uandikishaji wapigakura ilishajulikana muda mrefu.

“NLD tunasema mbinu hizo tumeshazigundua, NEC ifanye haraka kuandikisha wapigakura ili uchaguzi ufanyike Oktoba na si vinginevyo, ucheleweshaji huu wa makusudi utawagharimu,” alisema.

Fordia haioni dalili za uchaguziMkurugenzi wa Fordia, Buberwa Kaiza pia alisema haoni dalili za Uchaguzi Mkuu kufanyika mwaka huu kutokana na maandalizi yake kuchelewa.

Kaiza alisema ukata unaoikabili NEC na kuchelewa kwa maandalizi ya msingi ya utoaji wa elimu ya uraia, vinatoa picha kuwa mambo yanaenda mrama kuelekea Uchaguzi Mkuu.

“Nina shaka kuwa uchaguzi unaweza kuahirishwa kama ilivyotokea kwa shughuli ya Kura ya Maoni, kwa sababu naona maandalizi yamechelewa sana. Kwa kawaida, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu hufanyika mwaka mmoja na nusu kabla,” alisema Kaiza.

“Imebaki miezi mitano maandalizi hayajafanyika kikamilifu, sasa kama unataka kufanya uchaguzi huru na haki utawezaje kufanya maandalizi ya mwaka mmoja na nusu ndani ya miezi iliyobaki na wakati huo ukikabiliwa na uhaba wa fedha?”

Kitendo cha NEC kuchelewa kulipia mashine za BVR na kuziingiza nchini mashine hizo kwa awamu, kitafanya uandikishaji kuchelewa zaidi kwa kuwa mashine zilizopo ni moja ya nane tu ya mashine zote zinazotakiwa.

“Kwa vyovyote vile uandikishaji utakwenda hadi Oktoba kwa sababu ni mkoa mmoja tu wameshafanya hadi sasa, bado hawajafundisha wataalamu wa kuendesha mashine, hawajasafiri kwenda maeneo ya uandikishaji. Kuna matatizo ya kiufundi.

“Kwa namna gani wanaweza kufika mwezi Oktoba wakiwa wamemaliza kusajili, kuhakiki na kuthibitisha majina na NEC ikawa tayari kusimamia uchaguzi na mambo mengine?”


Mrema ataka uchaguzi uahirishwe
Hata hivyo, mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alikuwa na mtazamo tofauti ingawa anakiri kuwa maandalizi yanasuasua.

Mrema aliiambia Mwananchi jana kuwa katika mkutano uliofanyika Dodoma mwaka jana baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa upinzani chini ya mwamvuli wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), alishauri Uchaguzi Mkuu uahirishwe, lakini alitazamwa vibaya na viongozi wenzake wa upinzani.

“Wengine walihoji ‘huyu kibaraka anasema nini?’ Najua kuna ambao waliona huyu kikaragosi anataka kutuharibia mambo yetu,” alisema.

“Ambaye alinitazama vizuri ni Rais Kikwete pekee yake wengine wote walinitazama vibaya kabisa na nafikiri hata rais aliniona huyu naye sijui karogwa, lakini hakusema kitu,” alisema.Mbunge huyo wa Vunjo, alisema sasa kuna kila dalili kuwa uchaguzi mkuu kufanyika Oktoba ni jambo gumu.

“Nilisema siku hiyo na kupuuzwa, lakini hicho ndicho ambacho kinajitokeza sasa,” alisema na kuongeza kuwa mchakato wa uandikishaji katika Daftari la Wapigakura kwa teknolojia ya BVR umekwama.

Pia mchakato wa kuunda Katiba, nao huenda usikamilike kwa wakati na kwamba hata kama Kura ya Maoni itapigwa, itakuwa ngumu kwa taratibu zote kukamilika, ikiwa ni pamoja na marekebisho ya sheria na kanuni.

“Katiba ikipita kuna sheria na kanuni ambazo zitahitaji mabadiliko, wabunge ni lazima wakakutane kwa ajili hiyo hivyo sidhani kama muda utatosha hivyo ni wazi kuwa ili mambo yaweze kwenda sawa, ni lazima uchaguzi uahirishwe,” alisema.

Alisema, Rais Kikwete amechoka na kuwa katika nafasi hiyo urais ni jambo gumu, kuna changamoto nyingi na sasa angependa kupumzika.

Hata hivyo, alisema kabla ya kuahirisha Uchaguzi Mkuu, Serikali ni lazima ifanye majadiliano na wadau badala ya kukurupuka, kitu ambacho alisema kinaweza kusababisha mgogoro. “Wakiahirisha bila kushirikisha wadau, hasa (mwenyekiti wa DP, Christopher) Mtikila, wasubiri kesi Mahakama Kuu,” alisema.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company