Ukawa wavuruga Bunge Dodoma

> Wabunge wa Kambi ya Upinzani wa kundi la Ukawa wakijadiliana jambo bungeni jana baada ya kutaka bunge lisiendelee na kikao mpaka wapate majibu kutoka Serikalini kuhusu zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura (BVR). Picha na Anthony Siame
Na Fidelis Butahe na Sharon Sauwa

KWA UFUPI
Huku wakiwa wamesimama walikuwa wanapiga kelele wakisema, ‘hatutaki kuburuzwa’, ‘tumechoka kupelekeshwa’, Watanzania wapo njia panda’ na ‘tunataka majibu,’ ‘Bunge lisitumiwe kuilinda Serikali’, ‘Waziri Mkuu yupo bungeni kwa nini asitoe kauli’ na maneno mengine mengi bila mpangilio.
Dodoma. Wabunge wa upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana walianzisha tafrani bungeni na kusababisha kikao cha Bunge kuvunjika saa 5.18 asubuhi baada ya kusimama na kupaza sauti wakishinikiza Serikali itoe kauli juu ya hatima ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura na upigaji wa Kura ya Maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa.

Huku wakiwa wamesimama walikuwa wanapiga kelele wakisema, ‘hatutaki kuburuzwa’, ‘tumechoka kupelekeshwa’, Watanzania wapo njia panda’ na ‘tunataka majibu,’ ‘Bunge lisitumiwe kuilinda Serikali’, ‘Waziri Mkuu yupo bungeni kwa nini asitoe kauli’ na maneno mengine mengi bila mpangilio.

Wabunge hao wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF, kwa umoja wao walimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa majibu hayo muda huohuo, kabla ya jioni kutoa hutuba na kuahirisha mkutano huo wa 19 wa Bunge.

Baadaye jana usiku katika hotuba yake ya kuahirisha Bunge hadi Mei 12, utakapoanza Mkutano wa 20, Waziri Mkuu Pinda alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itatoa taarifa siku za hivi karibuni kuhusu upigaji wa kura ya maoni.

“Ni dhahiri muda uliobaki kuanzia sasa ni mfupi lakini Tume ndiyo itakayotujulisha ratiba kamili,” alisema.

Sakata lilivyoanza
Kelele hizo zilitokana na hoja za wabunge wawili, Suleiman Jafo wa Kisarawe na yule wa Ubungo, John Mnyika waliotaka Bunge lisitishe shughuli zake zote lijadili suala hilo kwa kuwa ni muhimu na Taifa halielewi hatima yake, wakati Bunge lilikuwa linaahirishwa jana.

Spika wa Bunge, Anne Makinda alikataa suala hilo kujadiliwa, akisema ni hoja iliyowasilishwa katika mkutano uliopita, akataka Bunge liendelee na shughuli zake, lakini wabunge wa upinzani walikataa kukaa na wakaendelea kupaza sauti.

Hata alipobadili kauli akasema, “nimesema kauli itatolewa, wabunge hao walisisitiza itolewe papohapo. Hata alipowataka waondoke ndani ya ukumbi huo, wabunge hao ambao ni wachache ukilinganisha na wale wa CCM, walikataa, wakisema; “hatutoki hadi kauli itolewe.”

Kelele za wabunge hao zilimfanya Spika Makinda kutoa kauli kali, “Njooni mwendeshe (kikao) nyinyi basi. Njooni hapa mkae tena wote.”

Baada ya kuona kelele hizo zimedumu kwa dakika tatu, Spika Makinda alilazimika kusitisha shughuli za Bunge hadi baadaye (jioni), bila kutaja muda ambao Bunge lingerejea na kuwaacha wabunge wakiwa wamesimama katika makundi ndani ya ukumbi wakijadili tukio hilo.

Jafo ndiye aliyeanza kuomba mwongozo wa Spika akitaka chombo hicho cha kutunga sheria kisitishe kujadili jambo lolote lile, badala yake kijadili mustakabali wa Katiba Mpya, akitaka Serikali iwasilishe muswada wa sheria kwenye mkutano wa 20 wa Bunge (wa Bajeti) ili Katiba ya Mpito ipitishwe.Jafo alitaka Katiba Inayopendekezwa ipitishwe kwa mpito ili kuondoa sintofahamu ya watu wanaotaka kuwapo mgombea binafsi, kupinga matokeo ya urais mahakamani, kuweka ukomo wa Bunge na wabunge na kuwapo kwa Tume huru ya uchaguzi.

Alisema mambo hayo manne ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele yamo katika Katiba Inayopendekezwa, hivyo ni vyema ikapitishwa kwa mpito ili mambo hayo tu manne yatumike katika Uchaguzi Mkuu.

Alisema wananchi wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura lakini kuna changamoto za upungufu wa vitendea kazi, zikiwamo mashine za kielektroniki za Biometric Voters Registration (BVR).

Alisema kutokana na hali hiyo, ni vigumu upigaji Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa.

Alisema upigaji kura ya maoni lazima utanguliwe na utoaji wa elimu kwa mpigakura, jambo ambalo kwa muda uliobaki ni vigumu kufanyika.

“Tutumie mkutano wa 20 tuhakikishe Serikali inaleta muswada wa hati ya dharura ili Bunge lipitishe katiba ya mpito, kwa sababu Taifa sasa hivi lipo katika hali tete kila mtu anasema lake. Endapo tutafanya hivyo tutakuwa na katiba ya mpito ya kati ya miezi sita hadi 12, itaturuhusu kufanya uchaguzi na baadaye watu watakwenda kwenye Kura ya Maoni wakiwa wamepata elimu ya kutosha juu ya Katiba Inayopendekezwa.”

Alisema uamuzi huo utalinusuru Taifa na si busara kuruhusu nchi kuingia katika kura ya maoni huku kukiwa na mvutano.
Baada ya kauli ya Jafo, Spika Makinda alisema: “Ulichokizungumza wala siyo utaratibu. Kwanza suala hilo litatolewa ufafanuzi jioni wakati Waziri Mkuu akiahirisha Bunge.”


Wakati Jafo akiomba mwongozo huo, Halima Mdee (Kawe - Chadema), John Mnyika (Ubungo - Chadema), Felix Mkosamali (Muhambwe - NCCR), Moses Machali (Kasulu Mjini - NCCR), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini - Chadema) na Mbatia walisimama bila kufuata utaratibu na kupaza sauti wakipinga mwongozo huo.

“Hivi huyu katumwa au nini. Anazungumza vitu gani humu ndani,” alisema Mdee na kuungwa mkono na Machali, huku wakitakiwa kukaa chini na Makinda.

Baada ya kutulia kwa mvutano huo uliodumu kwa takribani dakika nne, Mnyika aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya 47 (1) na kusema: “ Mpaka sasa uandikishaji wa wapigakura nchi nzima haujakamilika hata katika mkoa mmoja tu wa Njombe. Watanzania wapo katika sintofahamu kuhusu ni lini wataandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.”

Aliongeza, “Jambo hili ni la dharura kwa sababu limeshatolewa hoja ya dharura katika mkutano uliopita wa Bunge, ukaagiza (Spika) kamati ya bunge ilishughulikie, majibu yatolewe kwenye mkutano huu wa Bunge. Leo hii (jana) mkutano unakwenda kufungwa bila majibu kutolewa.”Mnyika alitaka shughuli zote za Bunge kwa siku ya jana zisitishwe na majibu juu ya masuala hayo mawili yapatikane.
“Nimeomba miongozo juu ya jambo hili mara mbili na mara zote Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu umeipa maelekezo ya kutoa majibu lakini inakwepa kutoa majibu,” alisema.

Alisema kwa mazingira hayo, hakuna sababu ya kuendelea na mjadala wowote katika kikao hicho cha Bunge mpaka majibu yapatikane, akisisitiza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya nchi, kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali.

Huku akimnyooshea kidole Pinda Mnyika alisema: “Waziri Mkuu (Pinda) yupo hapa anaweza kutoa majibu na tukajadili jambo hili.”

Baada ya Mnyika kuwasilisha mwongozo wake, Makinda alisema: “Hoja ya Mnyika inafanana na ile iliyotolewa na Jafo. Tuendelee Katibu (akielekeza kuendelea na ratiba za Bunge).”

Katibu wa Bunge alianza kusoma miswada minne iliyokuwa ikisomwa kwa mara ya kwanza, ikiwamo miwili ya habari na hapo ndipo wabunge hao wa upinzani waliposimama na kuanza kupiga kelele.

Wakiwa wamesimama, wabunge hao walianza kupaza sauti, akianza Machali ambaye aliwasha kipaza sauti kuwa, “Hoja hii haifanani kabisa na ile ya (Jafo), ile ya kwanza inataka majibu mkutano wa 20 na hoja hii ya pili inataka majibu katika kikao hiki cha leo”.

Majibizano
Mnyika: Hoja hii itolewe majibu na Waziri Mkuu yupo hapa. Atoe majibu

Machali: Tunataka majibu, tumechoka kuburuzwa.

Makinda: Anawaburuza nani, nimewaambia kwamba swali lile litajibiwa leo (jana) na Waziri Mkuu. Waziri kivuli njoo usome hotuba ya kambi ya upinzani.

Huku wabunge hao wakiwa bado wamesimama, Spika alimwita waziri kivuli wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, ili asome maoni ya kambi hiyo juu ya Mswada wa Sheria ya Miamala ya Kielektroni ya mwaka 2014 na ule wa Makosa ya Kimtandao wa mwaka 2015.Hata hivyo, msemaji huyo hakwenda kusoma maoni yake na badala yake wabunge hao waliendelea kusimama na kushinikiza kutaka majibu kutoka kwa waziri mkuu.


Baada ya kuona hali hiyo inaendelea, Makinda aliahirisha kikao hicho na kiliporejea saa 10 jioni, hoja hizo hazikuendelea, badala yake miswada iliendelea kujadiliwa. Habari zilizopatikana zilieleza kuwa Kamati ya Uongozi ilikutana na kukubaliana majibu yatolewe katika hotuba ya kuahirisha Bunge.

Nje ya ukumbi
Wakiwa nje ya Ukumbi wa Bunge, Mbunge wa kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia na mwenzake wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo walisema wanachokitaka kwa Serikali ni kauli tu juu ya suala hilo na si jambo jingine.

Tofauti na ilivyozoeleka kwamba wangeitana na kukaa kikao cha Kambi ya Upinzani, wabunge hao baada ya kutoka bungeni kila mmoja aliondoka zake, huku wakisikika wakiambiana, “Tukutane baadaye bungeni.”

Baadaye, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah alisema Bunge lingeendelea saa 10 jioni, huku akitupa lawama kwa upinzani kwamba walifanya makosa kugomea kuendelea kwa kikao cha Bunge, badala yake kama walikuwa na hoja walitakiwa kuiwasilisha kwa Spika.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company