VURUGU AFRIKA KUSINI: Membe asema hakuna Mtanzania aliyeuawa, 21 kurejea nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akizungumza na waandishi wa habari kuhusu vurugu zilizotokea nchini Afrika ya Kusini jijini Dar es Salaam jana.Picha na Said Khamisa
Na Peter Elias, Mwananchi
KWA UFUPI

Watu hao ambao ndiyo idadi ya Watanzania waliotambulika kuwa hatarini nchini humo, wanatarajia kuwasili nchini muda wowote baada ya Serikali ya Afrika Kusini kuridhia. Watakaorejea nchini ni Watanzania 21, wengine wawili wameomba kuendelea kubaki huko

Dar es Salaam. Watanzania 23 waishio Afrika Kusini wamewekwa kwenye kambi maalumu ya Isipingo nchini humo ili kupewa ulinzi wa maisha yao yaliyo hatarini kufuatia mashambulizi yanayofanywa na wazawa dhidi ya wageni.

Watu hao ambao ndiyo idadi ya Watanzania waliotambulika kuwa hatarini nchini humo, wanatarajia kuwasili nchini muda wowote baada ya Serikali ya Afrika Kusini kuridhia. Watakaorejea nchini ni Watanzania 21, wengine wawili wameomba kuendelea kubaki huko.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema hakuna Mtanzania aliyepoteza maisha katika vurugu zilizosababishwa na chuki dhidi ya wageni, lakini wapo Watanzania watatu waliokufa nchini humo kwa sababu nyinginezo.

Membe aliwataja waliofariki kuwa ni Rashid Jumanne. Alisema Mtanzania huyu alikuwa ni jambazi na aliuawa kilomita 90 kutoka mji wa Durban akiwa kwenye harakati zake za unyang’anyi.

Mtu wa pili alisema anaitwa Athman China. Alisema kijana huyu aliuawa kwa kuchomwa kisu ndani ya gereza la West Hill. Membe alifafanua kuwa China alifanya kosa la jinai akafungwa, na huko gerezani zikatokea fujo za wafungwa. Kijana huyo alikufa baada ya kuchomwa kisu na wafungwa wenzake.

Ally Mohamed alikuwa ni kijana wa tatu kufa akiwa Afrika Kusini. Membe alisema Mohamed alikuwa amelazwa hospitali huko Johanesberg kwa maradhi ya kifua kikuu. Kijana huyo alifariki baada ya kuugua kwa miezi miwili, na tayari mwili wake umewasili nchini kwa maziko.

“Kuna habari zimesambaa mitandaoni kwamba Watanzania wamekufa huko Afrika Kusini. Niweke wazi kuwa hakuna Mtanzania aliyepoteza maisha kutokana na vitendo vya chuki dhidi ya wageni. Mpaka sasa ni watu nane tu ndiyo waliopoteza maisha,” alisema waziri huyo na kuongeza kuwa watu hao wanatoka katika nchi za Ethiopia, Zimbabwe, Malawi na Swaziland.

Membe alisema aliwasiliana na Waziri wa Usalama wa Afrika Kusini, David Mahlobo akamthibitishia kuwa hakuna Mtanzania yoyote aliyekufa. Pia, alimwita balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ili aeleze zaidi madhara yaliyojitokeza kwa Watanzania waishio Afrika Kusini.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company