James Lembeli Aitaka Ikulu Imsafishe Pia Lowassa Kama Ilivyowasafishwa Watuhumiwa Wa Escrow.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Bunge kuchunguza madhara ya Operesheni Tokomeza, James Lembeli, amekosoa ‘mchezo mchafu’ wa serikali kuwasafisha baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali.


Amehoji kama suala ni kusafishana, kwanini juhudi kama hizo zisitumike kuwasafisha wengine pia kama Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa.


Lowassa alijiuzulu wadhifa wake kutokana na sakata la mtambo wa kufua umeme wa kampuni ya Richmond, mwaka 2007.

Wengine waliojiuzulu kufuatia sakata hilo ni Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi ambao wote walikuwa mawaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati tofauti wakati sakata hilo lilipoibuka bungeni mwaka 2008.

Akichangia hotuba ya mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2015/16 bungeni jana, Lembeli alisema, tabia hiyo italeta giza. Alisisitiza tabia ya kuwasafisha viongozi wachache na kuwaacha wengine ni mbaya.

“Kama kusafishana basi tusafishane wote na siyo watu wachache tu.
“Nchi hii sasa inaenda kubaya, watu wanawekwa kwenye makundi…kama kusafishana tusafishane wote na kama siyo hivyo huko tunakoenda kuna giza. Tabia iliyozuka sasa ya kusafishana na kuwaacha wengine ni mbaya,” alisema Lembeli ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.

Alisema licha ya kuwa alikuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la Richmond lililomlazimisha Lowasa ajiuzulu, kwa sasa haoni sababu za kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Monduli naye kutosafishwa.

Tokomeza
Alisema ripoti ya kamati yake ya Tokomeza, haikuwatia hatiani waliokuwa mawaziri watatu, Dk. Emmanuel Nchimbi-Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hamis Kagasheki-Maliasili na Utalii na Shamsi Vuai Nahodha- Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, isipokuwa waziri mmoja, Dk. Mathayo David Mathayo-Mifugo na Uvuvi.

“Nimeshtuka kusikia ripoti ya Tume ya Kimahakama ya Uchunguzi kuhusu sakata la Operesheni Tokomeza imesema mawaziri hao hawana makosa…kamati yangu iliweka bayana kwamba hao hawakuwa na makosa, kuna siri gani hapo,” alihoji na kuongeza:

“Lakini ripoti hiyo haizungumzii namna ya kuwalipa fidia ndugu wa watu waliokufa, waliojeruhiwa na kupata ulemavu au kuharibiwa mali zao.”

Alimtaja pia Ezekiel Maige, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, kwamba naye pia anahangaika na anastahili kusafishwa.

Tegeta Escrow
Kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, alisema, matokeo ya uchunguzi uliofanywa na serikali umewasafisha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi na kuwaacha wengine.

Alisema tatizo kubwa la sakata la Akaunti ya Escrow ni wale walioidhinisha fedha hizo kutolewa na siyo waliwekewa fedha kwenye akaunti zao. Kiasi cha Sh. bilioni 301 zilichotwa katika akaunti hiyo.

Alisema wakati akina Prof. Muhongo na Maswi wanasafishwa, akina Prof. Anna Tibaijuka wanahangaika kwa kutiwa hatiani na sakata hilo.

Alisema wakati Prof. Tibaijuka anahangaika kutokana na kuwekewa fedha kwenye akaunti yake, waliohusika kuidhinisha fedha hizo kutoka hawajachukuliwa hatua yo yote.

Alidai Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, naye anahangaika kwa kuwekewa fedha hizo, lakini kwa mujibu wa maelezo yake fedha hizo ni malipo ya kazi aliyokuwa ameifanya ya kutoa ushauri ambayo ni haki yake.


Ezekiel Wenje
Kwa upande wake, Mbunge wa Nyamagana, Ezakia Wenje, (Chadema), alirusha kijembe kwa watuhumiwa wa sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, akisema haiwezekani kwa mtu ambaye yumo kwenye ‘dili’ la kashfa za fedha asafishwe.

“Kosa la escrow ni wale walioidhinisha fedha hizo zitoke. Nikisikia mbunge yumo katika kila dili halafu anajisifia nje kuwa yeye ni ‘nyoka wa makengeza’ huyo huwezi kumsafisha,” alisema.

Sugu
Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi, amehoji sababu za serikali kununua magari 700 ya deraya na ya maji ya kuwasha badala ya kuipa fedha Tume ya Uchaguzi (NEC) isajili wapiga kura.

NEC iko taabani kifedha na imeshindwa kusajili wapiga kura na kununua vifaa vya kusajili kielektroniki (BVR).

Akiongea kwa mbwembwe na vibwagizo wakati wa kuchangia hotuba hiyo, Mbilinyi alisema inashangaza kuona kuwa hakuna kipaumbele. Alisema kati ya deraya (magari yasiyopenya risasi) 700 yanayonunuliwa anaomba 500 yapelekwe Mbeya ili wayafanyie kazi.

Sugu alisema wapinzani hawana ugomvi na serikali lakini wanachozungumzia ni masuala ya kutetea umma.

Alitoa mfano wa kura ya maoni wapinzani walisema haitafanyika, lakini serikali ikang’ang’ania kuwa itapigwa Aprili 30 jambo ambalo halikufanyika.

Aliongeza kuwa kuna msemo kuwa namba hazidanganyi, lakini watu huongopa hivyo serikali ya CCM ikubali kuwa hakuna sababu ya kuwadanganya wananchi kwa vile ukweli unaonekana.


“Wanawake au wanaume wanadanganya, lakini namba haziongopi 2+2 ni sawasawa na 4,” alisema Sugu na kutamba kuwa atashinda uchaguzi wa Oktoba.

Akizungumza kwa kuweka lugha za kimziki kama ‘yaah men’‘kamooni’ aliitaka CCM na serikali wasipate hofu (kupaniki) bali wawasikilize na wapinzani kwa vile nia ni kupeleka mbele maslahi ya nchi.

Mbunge mmoja alikifananisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ng’ombe anayesubiri kuchinjwa.


“CCM inaelekea kibla kama ng’ombe anayesubiri kisu, tumechoka tunataka kunufaika na rasilimali zetu. Ikifika Oktoba tunaichinja,”alisema Kuluthum Mchuchuri (CUF Viti Maalum).

Alisema Watanzania wanaishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu na si sera, bajeti wala mipango ya CCM.

Akitaja baadhi ya mambo yanayoipeleka CCM kibla ni pamoja kujenga maabara wakati hakuna walimu wa sayansi.

Alisema shule kama Mwara, Mwaseni na Umwe mkoani humo hazina walimu lakini maabara zinashinikizwa kujengwa.

Lakini pia vijembe viliendelea pale Zarina Madabida (Viti Maalum CCM), alipowafananisha wapinzani na wake wenza wa CCM, akisema hawawezi kuisifia CCM kwani kufanya hivyo ni sawa na mke mwenza kumsifia mwenzake.

Mbunge wa NCCR-Mageuzi Kasulu Mjini, Mosses Machali, alipinga kuwa serikali ya CCM haiwezi kujenga maabara bali ni wananchi ambao wanachangishwa fedha na wanashiriki kujenga majengo hayo.

Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan, aliulipua ujenzi wa barabara ziendazo haraka jijini Dar es Salaam (Dart) kuwa ni chanzo cha mafuriko.

Alisema barabara hizo zimegeuza Jangwani kuwa uwanja wa mafuriko na kusababisha maji kujaa juu ya barabara kutokana na ujenzi na vifusi vilivyomwagwa.


Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema, alisema siasa zinazotumia propaganda za udini na ukabila zinatumika kuichafua Chadema.

Aliyasema hayo kufuatia maelezo ya Mohamed Amour Chombo (CCM) Magomeni, aliyesema Ukawa wanashangaza kudai wataondoa ubaguzi wakati ndiyo vinara wa kubagua.

Chombo alieleza kuwa Cuf ni wabaguzi kwa asilimia 100, akitaja kuwa huko Pemba kiongozi akiomba uongozi hawezi kupewa kama anatokea Unguja.

Na hata Unguja ndicho wanachofanya ni wabaguzi na wanachaguana kwa misingi ya U-Cuf na Upemba.

Aliendelea kusema kuwa, kwa Chadema mtiririko wa uongozi wao unaonyesha jinsi walivyo watu wa eneo moja, baada ya kumaliza maelezo hayo ilifika fursa ya Lema kuchangia na akasema Chombo anastahili kupigwa risasi.

Akimshambulia zaidi, alisema ingekuwa ni Korea Kaskazini mbunge kama huyo Waziri wa Ulinzi, angeamuru apigwe risasi.

Alionya kuwa kuendelea kuendesha nchi kwa utaratibu wa udini na ukabila kutasababisha taifa kuparaganyika.

Waziri wa zamani wa elimu, Prof. Athumani Kapuya, ametahadharisha kuwa sera ya elimu inayoelekeza Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia taasisi zote za elimu itahatarisha amani ya taifa.

Alisema sera ya elimu itateketeza amani ya Tanzania na kwamba yanahitajika mapinduzi ya elimu.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company