Mwandamanaji nchini Burundi
REUTERS/Goran Tomasevic
Na Emmanuel Richard Makundi
Jaribio la kutaka kumpindua rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza limeshindikana wakati huu ambapo kiongozi aliyekuwa akiongoza harakati hizo, kukubali kuwa ameshindwa ambapo baadhi yao wamelazimika kukimbia na wengine kujisalimisha kwa vyombo vya usalama.
Hatua hii imekuja baada ya wanajeshi walioasi kuzidiwa uwezo na wanajeshi watiifu kwa Serikali ya rais Nkurunziza, ambapo toka juzi walikuwa wanawania kuchukua kituo cha taifa cha Televisheni na Redio.
Jenerali Godefroid Niyombare ambaye alianzisha jaribio la kutaka kufanya mapinduzi mwanzoni Jumatano ya wiki hii, ameliambia shirika la utangazaji la Ufaransa, kuwa alitaka kujisalimisha huku baadhi ya wasaidizi wake wakikamatwa.
Jaribio hili la aina yake, limemalizika ndani ya saa 48 baada ya hapo awali kuwepo taarifa kuwa haijulikani ni nani hasa ambaye alikuwa anaumiliki wa Serikali baada ya kushuhudia maandamano ya wananchi wanaopinga rais Nkurunziza kuwania muhula watatu wa urais.
Jenerali Niyombare, anasema kuwa "Tumeamua kujisalimisha, na nimatumaini yetu kuwa hawatatuua". Alisema Niyombare.
Kiongozi mmoja wa juu wa Polisi nchini Burundi, amethibitisha kujisalimisha kwa wanajeshi hao, ambapo ameongeza kuwa jenerali Niyombare pamoja na wanajeshi wengine wanaomuunga mkono wamekimbia na wanatafutwa.
Hali ilivyokuwa Burundi, May 14, 2015REUTERS/Goran Tomasevic
Msemaji wa jenerali Niyombare, Zenon Ndabaneze akizungumza na shirika la habari la AFP amethibitisha wanajeshi wao kujisalimisha baada ya yeye mwenyewe kukamatwa na wanajeshi wa Serikali, ambapo pia naibu wake Niyombare, Cyrille Ndayirukiye na wenzake wengine pia wamekamatwa.
"Tumeamua kujisalimisha, tumeweka chini silaha zetu, tumewapigia simu wizara ya mambo ya ndani kuwataarifu kuwa hatuna silaha tena". Alisema Ndabaneze saa chache kabla ya kukamatwa kwake.
Mwandishi wa rfi idhaa ya kiingereza, Danniel Finnan aliyeko mjini Bujumbura, Burundi, amesema kuwa hali kwa sasa imerejea kwenye hali yake ya kawaida licha ya maandamano ya hapa na pale katika baadhi ya maeneo, ambako pia kumesikika milio ya risasi.
Katika hatua nyingine, msemaji wa rais Nkurunziza, amethibitisha kuwa kiongozi wake amerejea mjini Bujumbura usiku wa kuamkia leo na kwamba leo Ijumaa anatarajiwa kulihutubia taifa kupitia njia ya televisheni.
Wakati jaribio hili linafanyika, rais Nkurunziza alikuwa nchini Tanzania, ambako alienda kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na kati, lakini akashindwa kushiriki baada ya kupokea taarifa za jaribio la mapinduzi.
Wanajeshi wanaomuunga mkono rais Nkurunziza wakiwa wanafanya doria mjini BujumburaREUTERS/Goran Tomasevic
Taarifa zaidi kutoka jijini Bujumbura zinasema kuwa mashirika ya kiraia yametoa wito kwa wananchi kujitokeza tena barabarani kushiriki kwenye maandamano zaidi ya kupinga rais Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Machafuko yaliyoshuhudiwa nchini Burundi kwa takribani majuma matatu sasa, yametokana na hatua ya rais Nkurunziza kutangaza kuwania urais kwa muhula wa tatu licha ya shinikizo la kimataifa kumtaka asigombee.
Juma hili wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini dar ee Salaam, Tanzania, walilaani mapinduzi yaliyofanyika nchini Burundi, na kutaka uchaguzi mkuu usogezwe mbele na pia kuheshimiwa kwa mkataba wa Arusha unaotaka rais wa Burundi kuwania urais kwa mihula miwili pekee.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago