Wahamiaji wa kabila la Rohingya kutoka Myanmar |
Misaada ya kibinadamu kadhalika itatolewa kwa uchukuzi wa barabarani na majini, amesema waziri mkuu Razak.
Tangazo lake limekuja baada ya maafisa kuzuia mashua za wahamiaji hao kuingia katika maji ya Malaysia, na wakati mwingine kuziondoa kwa kuzikokota kutoka maji hayo kwa majuma kadhaa.
Mawaziri wa mashauri ya nchi za Kigeni wa Malaysia na Indonesia wamo nchini Myanmar kwa ajili ya mazungumzo kuhusu tatizo hilo la wahamiaji. Takriban watu 7,000 wanaaminika kuwa wamekwama baharini.
Wahamiaji hao wanajumuisha Waislamu wa kabila la Rohingya wanaotoroka mateso pamoja na kuhangaishwa nchini Myanmar. Wapo pia raia wa Bangladesh, ambao wanadhaniwa kuwa wahamiaji wanaotafuta hifadhi ya kiuchumi.
Malaysia pamoja na Indonesia zimesema kuwa zitatoa hifadhi ya muda kwa wale watakao wasili katika maeneo yao, lakini zinahitaji msaada kutoka jamii ya kimataifa kuwasaidia kuwapa makaazi.
'Nipe nikupe'
Katika mtandao wake wa Twitter Bw. Najib amesema kimsing "ni swala la huruma ya kibinadamu" kutoa msaada kwa watu walio na njaa pamoja na magonjwa. Ameongeza kusema kuwa operesheni ya kuwatafuta na kuwaokoa itakayoendeshwa na manowari za taifa hilo inahitajika ''ili kuepuka vifo''.
Malaysia ilikuwa miongoni mwa nchi kadhaa katika eneo hilo la Asia kukataa kuwapokea wahamiaji na imekuwa ikikokota mashua zao hadi katika maji ya nchi nyingine, katika kile wadadisi wamelaani kama ''mchezo hatari wa nipe nikupe''.