Wananchi Sengerema Wampa BARAKA Ngeleja Kugombea Urais.......Wasema Jina Lake Likikatwa Arudi Agombee Ubunge

WAKAZI wa Vijiji vya Nyabila na Sigu, Jimbo la Sengerema, mkoani Mwanza, wamemuomba Mbunge wao, Bw. William Ngeleja kuwania nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Wamesema kama jina lake litakwama kupitishwa ndani ya chama, watamchagua kwa mara nyingine ili aendelee kuwa mbunge wao kwa kipindi cha miaka mitano kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi.

Wakazi hao waliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Nyabila, baada ya Bw. Ngeleja kuzindua miradi miwili ya maji katika vijiji hivyo yenye thamani ya sh. milioni 18 ambazo zimetolewa na Mfuko wa Jimbo ambao mbunge huyo ndiye Mwenyekiti wake.

''Pamoja na kwamba bado hujatangaza rasmi nia ya kugombea nafasi nyeti ya urais ili kurithi mikoba ya Rais Jakaya Kikwete, sisi tuna imani kubwa na utendaji wako na kuona unafaa kuwa Rais wa Awamu ya Tano," alisema mkazi mmoja wa Kijiji cha Nyabila ambaye aliungwa mkono na umati mkubwa wa watu waliokuwepo katika mkutano huo.

Baada ya mkutano huo, Bw. Ngeleja na msafara wake walikwenda Kijiji cha Kagunga kuzindua kisima kilichojengwa katika kitongoji cha Sigu na kupewa baraka kama alizopewa Kijiji cha Nyabila baada ya wananchi kumtaka agombee urais na asipoteuliwa basi agombee ubunge wa jimbo hilo.

"Mheshimiwa Mbunge, wananchi wa Kagunga tunakutaka tena uchukue fomu ili nasi tuonyeshe shukurani zetu kwako, kwa kauli moja tuko tayari kulipa gharama za fomu ya kugombea tena ubunge katika jimbo la Sengerema," walisema wakazi hao katika risala yao kwa mbunge huyo.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company